KIUNGO wa timu ya taifa ya Tanzania, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ana imani kikosi hicho kitafikia malengo katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 nchini Morocco.
Fei Toto anaamini Taifa Stars itaendeleza kiwango chake katika michuano hiyo kama ilivyokuwa kwenye Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) na kwa mara ya kwanza ilitinga hatua ya mtoano.
“Kila mtu ana ari baada ya kile tulichokifanya kwenye CHAN. Hiyo ilikuwa michezo migumu sana ambayo ni karibu sawa na AFCON. Lakini hii itakuwa ngumu zaidi kwa sababu tunashindana na wachezaji bora zaidi barani Afrika kutoka duniani kote,” Fei Toto alisema.
“Lakini, tumejenga imani ya ajabu na ari ya kupambana kutokana na kile tulichokifanya kwenye CHAN. AFCON ni moja ya mashindano makubwa duniani na hatua ambayo kila mchezaji anataka kung’ara.
“Ni sawa na sisi; tunataka kuipigania nchi yetu. Tumejiandaa vyema na tayari kwa kile kilicho mbele yetu. Tuko kwenye kundi gumu sana lakini tunatarajia kucheza katika kiwango bora. Tunapaswa kuwa tayari kushindana.”
Kuhusu kufanya kazi chini ya Miguel Gamondi ambaye anakaimu nafasi ya kocha mkuu baada ya kuondoka kwa Hemed Suleiman, kiungo huyo alisema: “Tumejifunza mengi hasa kutoka Ivory Coast mara ya mwisho, tunatakiwa kujitoa asilimia 100 katika kila mchezo, kuna nafasi ndogo sana ya kufanya makosa na lazima ucheze kwa nidhamu ya hali ya juu.
“Kutokana na tulichojifunza, tunataka kufanya vizuri zaidi na kuna imani katika kundi kwamba tunaweza kufikia lengo letu. Tuna kikosi chenye nguvu sana cha kucheza na kocha Gamondi mwenye uzoefu, tunaamini hii ni njia sahihi kwetu kufanya vizuri.”
Katika CHAN 2024 ambapo Tanzania ilikuwa mwenyeji kwa kushirikiana na Uganda na Kenya, ilitinga robo fainali ya michuano hiyo iliyofanyika Agosti 2025, ikaenda kupoteza mbele ya Morocco iliyokuja kufika hadi fainali na kubeba ubingwa.
Kwa upande wa AFCON 2025, Taifa Stars imepangwa kundi C na timu za Nigeria, Uganda na Tunisia, huku fainali zilizopita zilizochezwa mwaka 2024 nchini Ivory Coast, Taifa Stars ilipangwa kundi F, ikamaliza mkiani na pointi mbili sawa na Zambia, huku DR Congo (3) na Morocco (7) zikisonga hatua inayofuata kwa kushika nafasi mbili za juu.