Dar es Salaam. Mwanadiplomasia Mwandamizi, Omar Mjenga, amewataka wahariri wa vyombo vya habari kuwa chimbuko la hoja na mijadala mipana kuhusu umuhimu wa kulinda amani na masilahi ya Taifa, hasa ya jamii inapotofautiana kimtazamo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Desemba 23, 2025, wakati akiwasilisha nasaha na uzoefu wa wazee, katika semina ya wahariri iliyobeba mada ya ‘Wajibu wa vyombo vya habari katika kulinda Muungano, Mjenga amesema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuimarisha umoja wa kitaifa na kulinda misingi ya amani.
Mkutano huo umefunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni.
Mjenga amewataka wahariri kutokuwa waoga katika kusimamia ukweli na masilahi ya Taifa, akiwasisitiza wavuke mipaka ya woga na masilahi binafsi wanapotekeleza majukumu yao ya kihabari.
“Wahariri wa habari msijishushe wala kujifungia nyumbani. Vukeni mipaka, lakini mtambue kuwa umoja wetu ndiyo fahari yetu. Kila unachoandika kinapaswa kupimwa kwa kuangalia athari zake kwa Taifa,” amesema Mjenga.
Amesema katika mazingira ya sasa, usalama wa nchi unaweza kuvurugika kwa urahisi endapo tahadhari haitachukuliwa, hivyo ni muhimu kwa waandishi na wahariri kutambua ipasavyo nini cha kusema na cha kunyamaza kwa masilahi mapana ya nchi.
Mjenga ameeleza wasiwasi wake juu ya baadhi ya waandishi kushirikiana na wenzao wa nje bila kuzingatia athari kwa masilahi ya Taifa, akisisitiza vyombo vya habari vijikite kwanza katika kulinda Muungano na umoja wa kitaifa.
Amewataka wahariri kuendelea kuelimisha umma kuhusu uzalendo, ubora wa uandishi, habari za uchunguzi na haki hususan katika vipindi vya chaguzi.
“Inafahamika kuwa wakati mwingine waandishi hulipwa ili kumchafua mgombea fulani. Tendeni haki. Acheni kupamba habari za uongo kuwa za kweli, au kuandika habari za kweli kwa kuzipindisha hadi zionekane za uongo,” amesema.