Madereva wamulikwa kuelekea mwishoni mwa mwaka

Arusha. Kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, madereva wakiwamo wa mabasi ya abiria, wametakiwa kuzingatia sheria za barabarani ili kuepuka ajali na kuokoa maisha.

Mbali ya hayo, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limeendelea kutoa elimu kwa madereva hao na kufanya ukaguzi, lengo likiwa kuhakikisha usalama barabarani unakuwepo wakati wote.

Hayo yamesemwa usiku wa kuamkia leo Jumanne Desemba 23, 2025 na Mkuu wa Operesheni wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Joseph Mwakabonga, alipozungumza na baadhi ya madereva wa mabasi hayo katika eneo la Kikatiti, Barabara Kuu ya Moshi-Arusha.

Amesema ukaguzi huo ni mwendelezo wa operesheni zinazoendelea kufanyika katika barabara kuangalia hali halisi ya magari yanavyosafirisha abiria nyakati za usiku.

“Abiria wengi wanapenda kusafiri usiku, hivyo tumeona ni muhimu na sisi tukaenda nao sambamba ili kujua changamoto zinazokuwepo nyakati za usiku,” amesema.

Mwakabonga amesema walichobaini ni kuwa, baadhi ya mabasi yanajaza abiria kupita kiasi, mengine yanakwenda mwendokasi kinyume cha sheria.

Amesema waliokutwa wamepakia abiria waliozidi zaidi ya uwezo wa gari wamechukua hatua na kwamba, wengine hawatoi tiketi kama ilivyoelekezwa na sheria.

Ametaja baadhi ya hatua hizo ni kuwashusha abiria waliozidi, kuwarudishia nauli zao ili watafute usafiri mwingine, huku mamlaka ya Latra (Mamlaka y Udhibiti wa Usafiri Ardhini), ikiwatoza faini hao na waliozidisha mwendo.

“Lawama zimekuwa nyingi kwa madereva hawa wa mabasi kuwa ni wakiukaji wakubwa wa sheria za usalama barabarani na wamekuwa wakifanya vurugu nyingi za uvunjaji wa sheria,”amesema na kuongeza:

“Natoa wito kwa madereva wa mabasi tufuate sheria za usalama barabarani na kanuni zinazotuongoza ili abiria wanaosafirishwa katika mabasi hayo waende salama katika safari zao bila kupata changamoto yoyote.”

Amesema operesheni hiyo ni endelevu usiku na mchana na wataendelea kufuatilia magari barabara zote, wakihama eneo moja hadi lingine ili kuhakikisha madereva wanafuata sheria na kanuni.

Pia, ameeleza jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua wanaokiuka sheria.

Abiria aliyekuwa akielekea jijini Dar es Salaam, Neema Julius, amesema ni muhimu operesheni hizo kuwa endelevu kwani zitasaidia kupunguza ajali.