Tume ya Utumishi yakubali rufaa 15, ikitaja makosa matano kinara

Dodoma. Tume ya Utumishi wa Umma (TUU) imekubali rufaa 15 kati ya 88 zilizoombwa, ikitaja makosa matano yanayolalamikiwa zaidi.

Makosa hayo ni utoro kazini, wizi na rushwa kwa mali ya umma, kughushi vyeti na taarifa za uongo, kukiuka maadili, uzembe uliosababisha hasara kwa Serikali na uzembe wa kushindwa kutekeleza majukumu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumanne Desemba 23, 2025, Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso, amesema makosa hayo yamebainika katika mkutano wa pili uliomalizika hivi karibuni mjini Morogoro.

Huu ulikuwa mkutano wa pili kwa mwaka huu wa fedha ambao ulifanyika Manispaa ya Morogoro chini ya Mwenyekiti wake Jaji mstaafu Hamisa Kalombola.

Mbisso amesema makosa hayo yalichomoza kwa wingi kwenye malalamiko, hivyo yalionekana kutendwa zaidi na watumishi wa umma.

“Kwa upande wa malalamiko, mengi yaliyowasilishwa na kuamuliwa na Tume yalihusu kupinga watumishi kutolipwa stahiki zao na waajiri, ikiwemo mishahara, stahiki za uhamisho na posho mbalimbali zitokanazo na kutekeleza majukumu yao,” amesema.

Ametaja malalamiko mengine ni kuondolewa kwenye utumishi wa umma kinyume cha sheria na kusitishwa kwa ajira kinyume cha sheria.

Mbisso amesema watumishi 15 rufaa zao zilishinda moja kwa moja, wakati 14 walikubaliwa kwa masharti maalumu.

Kwa idadi hiyo, jumla ya watumishi 49 wamenufaika kwa mwaka huu wa fedha kurudishwa kazini, waajiri wakiagizwa kutoa haki kwa watumishi hao, ikiwamo kulipwa stahiki zao.

Ofisa wa Tume ya Utumishi wa Umma, Hussein Mussa amesema watumishi 15 si kwamba wote walikuwa wamefukuzwa na waajiri wao bali ndani ya rufaa hizo wengine walikuwa na rufaa za kuondolewa madaraja na kusimamishiwa mishahara.

Amesema siyo rufaa zote zinazopelekwa mbele ya Tume ni za watu kufukuzwa kazi, kwani wengine hupeleka malalamiko kutokana na kupunguziwa mishahara, kushushwa vyeo na wengine kuwa na barua za onyo bila sababu za msingi.

“Kwa hiyo tunaposema rufaa zimekubakiwa ni pamoja na makundi hayo na kwa namna yoyote mtu akishinda inabidi arudishiwe haki na stahiki zake zote ambazo alishazipoteza au kunyang’anywa,” amesema.