Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka wananchi kukubali mabadiliko na kuondoa hofu ya kudhulumiwa kupisha maeneo yao ya kale ili ijengwe miji ya kisasa.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Desemba 23, 2025 alipozindua nyumba za gharama nafuu za makazi na biashara zilizojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), katika mji wa Dk Hussein Mwinyi, Mombasa, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Uzinduzi huo ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar zinazotarajiwa kufanyika Januari 12, 2026.
Dk Mwinyi amesema mara nyingi wanapotaka kujenga nyumba za kisasa na kuendeleza miji kumekuwa kukiibuka hofu miongoni mwa wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo yanapaswa kuendelezwa.
“Tunapotaka kujenga nyumba mpya katika maeneo ya Michenzani, Kilimani, Kwahani na mengine hofu zinaingia, hatuna sababu ya kujenga hofu hakuna atakayedhulumiwa, kila mmoja atapata haki yake lakini ni vyema tukakubali kupisha maeneo hayo kwa ajili ya maendeleo na kuendeleza miji yetu,” amesema.
Amesema lengo la Serikali ni kuona Zanzibar nzima ikiwa na malengo ya kisasa ili kutimiza mipango na watakapoondoka madarakani waache alama isiyofutika.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akikata utepe kuashiria uzinduzi wa nyumba 276 za biashara na makazi mji wa Dk Hussein Mwinyi Mombasa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Licha ya kuipongeza ZSSF kwa kazi wanayoifanya, ameutaka mfuko huo kuanzisha miradi mikubwa zaidi ya majengo ikiwamo ya umeme.
“Ningependa kuona ZSSF mkifanya miradi mikubwa mikubwa, mfano hapa Zanzibar tuna changamoto ya umeme, kwa hiyo twende kuwekeza huko. Napenda kuona Zanzibar inabadilika kwa maendeleo, sioni sababu kwa nini ZSSF tusifikie huko,” amesema.
Dk Mwinyi amesema duniani kote mifuko ya hifadhi ya jamii ndiyo inaleta maendeleo kwa kujenga miundombinu mikubwa katika nchi zao kupitia fedha wanazohifadhi za wanachama wake.
Akitoa mfano wa nchi za Singapore na Malaysia namna zimeendelea katika ujenzi wa miradi ya majengo makubwa na mingine, Dk Mwinyi amesema hakuna sababu Zanzibar isifikie huko.
Pia, amezitaka taasisi zingine ambazo zinamiliki maeneo lakini hazina uwezo wa kuyaendeleza kwa miradi mikubwa, kuyatoa kwenye taasisi za uwekezaji, ambapo wao watanufaika na nchi itanufaika kwa miradi mikubwa.
“Niwapongeze umoja wa watu wenye ulemavu ambao walitoa eneo hili, wangeweza kukataa lakini kwa kuona umuhimu wamelitoa, wamenufaika na nchi itanufaika, hivi ndivyo tunavyotaka. Kwa hiyo, nitoe wito kwa taasisi zingine zenye maeneo kufanya hivyo,” amesema.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Rahma Salim Mahfoudh, amesema yamejengwa majengo 14 ya ghorofa nne sawa na nyumba 276 kwa gharama ya Sh34.163 bilioni.
Mradi huo wa miaka miwili umejengwa na Kampuni ya CRJE ya nchini China. Mkataba wa mradi huo ulianza mwaka 2022 na ulitakiwa kukamilika Desemba 2024 lakini kutokana na changamoto ya mitaro katika eneo hilo mkandarasi ameongezewa miezi sita.
Eneo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 22,500, lilikuwa likimilikiwa na Umoja wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar, lililipiwa fidia ya Sh1.7 bilioni na ZSSF kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.
Kwa mujibu wa katibu mkuu, mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa Sh24.1 bilioni sawa na asilimia 82 ya fedha zote.
Nyumba hizo zipo zenye vyumba kati ya viwili hadi vinne.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF, Nassor Shaaban Ameir, amesema wameuza nyumba hizo za bei nafuu kwa fedha taslimu, awamu na kupitia benki.
Amesema nyumba hizo zimeuzwa bila kuwapo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambapo asilimia yake imelipwa na Dk Mwinyi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Akil amesema watajitahidi kutunza na kuendeleza aliyoyaanzisha Dk Mwinyi ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yakifikiwa.
