Dar es Salaam. Unaweza kueleza kuwa, jitihada za kuhamia matumizi ya nishati safi ya kupikia zimeanza kuzaa matunda baada ya Tanzania kushuhudia kupungua kwa fedha zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi.
Ripoti ya tathmini ya hali ya uchumi ya kila mwezi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Novemba 2025, inaonyesha fedha zilizotumika kuagiza mafuta zilifikia Sh5.95 trilioni katika mwaka ulioishia Oktoba, 2025 zikipungua kutoka Sh8.304 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2022, sawa na asilimia 28.34.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali hiyo ilichangiwa na kupungua kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia kunatokana na ziada ya usambazaji na mahitaji hafifu.
Vilevile, bei za bidhaa za petroli zikijumuisha petroli, dizeli na mafuta ya taa ziliendelea kupungua Oktoba 2025, katika soko la dunia.
Uagizaji wa mafuta ulipungua kwa asilimia 12.5 na kufikia Dola 2,394.4 milioni za Marekani, uliochangiwa zaidi na kushuka kwa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia.
Hata hivyo, hali hiyo inaelezwa na wachambuzi wa uchumi, kuwa imechochewa na kuwapo ongezeko la vyombo vya moto na viwanda vinavyotumia gesi na umeme, hivyo kupunguza matumizi ya mafuta.
Kwa upande mwingine, hali hiyo imetajwa kuwa ni fursa muhimu kwa kuwa inaongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja, kuzalisha ajira na kupunguza uzalishaji hewa ya ukaa.
Akizungumzia hali hiyo, Dk Eliaza Mkuna, mtaalamu wa uchumi na biashara amesema kupungua kwa uagizaji wa mafuta ni fursa mpya inayotengenezwa ya kuwapo mahitaji ya nishati mbadala ya kuendesha viwanda, magari na hata pikipiki za matairi matatu.
“Siku hizi kuna pikipiki nyingi za matairi matatu za umeme, kuna ongezeko la magari ya umeme na jitihada za Serikali za kutengeneza vituo vya kuuza gesi zinazoendelea katika maeneo mbalimbali, ni kuonyesha fursa iliyopo,” amesema.
Amesema ongezeko la matumizi ya nishati mbadala katika maeneo mbalimbali, linaongeza fursa za ajira na kipato kutokana na kutumia nishati nafuu katika uendeshaji.
“Kama mtu anafanya biashara, basi atakuwa akitumia fedha kidogo kuweka nishati ya gesi na anapata faida kubwa, inaongeza kipato cha mtu mmoja mmoja,” amesema.
Amesema ongezeko la vituo vya kujaza gesi limeongeza ajira kwa watu wanaotoa huduma, huku mazingira yakilindwa kutokana na kupungua kwa hewa ukaa inayozalishwa.
“Hii inatusaidia kuepukana na magonjwa yanayoambukizwa na hewa ukaa… hivyo hii inaleta faida kwa mtu mmoja mmoja kwa kutumia nishati za bei nafuu na mazingira kutunzwa, hivyo inasaidia kuokoa gharama ambazo tungeweza kutumia katika kutibu magonjwa,” amesema.
Mtazamo huo unaungwa mkono na ongezeko la takwimu za mtandao wa usambazaji gesi asilia nchini kutoka kilomita 102.54 mwaka 2020/21 hadi kilomita 241.58 Aprili 2025.
Mtandao huo umewezesha kuunganishwa kwa jumla ya nyumba 1,514, taasisi 13 na viwanda 57.
Zaidi ya vyombo vya moto 15,000 vinatumia gesi asilia (CNG) hali iliyopunguza mahitaji ya petroli na dizeli katika uendeshaji wa vyombo hivyo nchini.
Kwa upande wake, Dk Lutengano Mwinuka kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema hali hiyo pia inaweza kuchangiwa na kuimarika kwa Shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni, ambayo inaifanya kuwa na nguvu katika ununuzi.
“Kama Shilingi imeimarika unaweza kununua vitu vingi kwa fedha kidogo kwa sababu unapobadili fedha unatumia hela kidogo kupata bidhaa nyingi za fedha za kigeni,” amesema.
Amesema ununuzi wa mafuta kwa pamoja unaweza kuwa na faida kwani unawezesha nchi kuwa na akiba ya muda mrefu na kama yalinunuliwa wakati ambao bei ni ndogo inaleta ahueni.
“Lakini pia kuna vyombo vya moto baadhi vinahamia katika matumizi ya gesi kutoka katika mafuta, japokuwa hii ni vigumu kuihesabu kwa sababu kuna magari mapya ya mafuta pia yanaletwa, hivyo yanaongeza mahitaji,” amesema.
Bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2025/2026 inaonyesha hadi kufikia Aprili 2025, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitoa vibali 10 vya ujenzi wa vituo vya gesi asilia (CNG) katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Ewura pia ilitoa leseni tano za uendeshaji vituo vya CNG na vibali sita vya ujenzi wa mabomba ya kupeleka gesi asilia kwenye viwanda, taasisi, migahawa ya chakula na majumbani.
Kati ya vibali hivyo, kibali kimoja kilitolewa kwa Kampuni ya PAET kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kupeleka gesi asilia kwenye kiwanda cha Aluminium Africa (ALAF) jijini Dar es Salaam na vinne kwa Kampuni ya TPDC kwa ajili ya kuunganisha gesi asilia kwenye nyumba 451 katika maeneo ya Mnazi Mmoja (Lindi), nyumba 529 maeneo ya Mkuranga (Pwani), Mlimani City Mall na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce).
