Wahariri wapewa elimu kuhusu Muungano

Mwandishi Wetu

Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamadi Yussuf Masauni amesema Waandishi wa Habari wana wajibu mkubwa katika kusimamia uwepo wa taarifa zinazojenga Muungano na kuondoa upotoshaji unaoweza kusababisha mgawanyiko.

Mhe. Masauni amesema vyombo vya habari vina umuhimu wa kuhakikisha taarifa zinazochapishwa ni sahihi, zenye vyanzo vya kuaminika, kuandaa mijadala yenye tija, isiyo na jazba wala kuchochea mgawanyiko, kuangazia mafanikio ya Muungano badala ya kusubiri tu changamoto.

Ameyasema hayo Disemba 23, 2025 wakati akifungua Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa kwa kuwataka kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kikatiba, historia, na faida za Muungano pamoja na kutoa jukwaa la uwiano, linalosikiliza sauti zote bila kujenga uadui.

“Wahariri wa Vyombo vya Habari, kufuatilia kwa makini mada zitakazotolewa na wabobezi wetu wa masuala ya Muungano ili zitujengee weledi katika uandishi wa taarifa zinazohusu Muungano kwa maslahi mapana ya Taifa letu na mustakabali wa Muungano wetu adimu na adhimu”

“Mkakati huo unalenga kuhakikisha kizazi kipya kinatambua thamani ya urithi huo wa kihistoria, huku hatua kali za kisheria zikitajwa dhidi ya watu wanaojihusisha na hujuma au uharibifu wa misingi ya Muungano.

Amesema Ofisi imeandaa programu maalum zitakazokuwa vivutio kwa vijana, ikiwemo michezo na sanaa, ili kujifunza historia ya nchi yao. Pia, kutakuwa na utaratibu wa wanafunzi kutembelea maeneo ya kihistoria na kuanzishwa kwa chaneli mahususi itakayozungumzia masuala ya Muungano pekee.

Aliongeza kuwa ukosefu wa uelewa miongoni mwa vijana ni changamoto inayopaswa kutatuliwa ili waweze kuenzi misingi ya nchi bila kuyumbishwa na mabadiliko ya teknolojia au upotoshaji wa mitandaoni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema ni vyema bajeti ya kutosha ikatengwa ili kuwezesha vyombo vya habari kutoa elimu ya muungano ipasavyo.

Amesema vyombo vya habari vikipewa bajeti ya kutosha itafanya kazi vizuri katika utoaji wa elimu na kuisaidia jamii kujifunza kwa wingi kuhusu umuhimu wa Muungano kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Afya Muhimbili (MUHAS), Dk. Harrison Mwakyembe, alisema kuijua vizuri historia kutasaidia jamii kuepukana na upotoshaji unaoweza kuhatarisha mustakabali wa nchi.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Abdallah Mkumbukwa, alieleza upekee wa Muungano wa Tanzania akilinganisha na mataifa kama Misri na Syria au Ghana na Guinea ambayo yalishindwa kudumisha miungano yao.

“Muungano wetu uliasisiwa kwa amani na makubaliano, si kwa shinikizo la wakoloni. Umehifadhi utambulisho wa pande zote na umekuwa chachu ya amani na utulivu katika kanda ya Afrika Mashariki,” alisema Dk. Mkumbukwa.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano Mstaafu Ofisi ya Rais (Ikulu), Salvatory Rweyemamu, aliwakumbusha waandishi kupunguza ushabiki wanapoandika habari za Muungano, huku Mwanadiplomasia Mwandamizi, Omar Mjenga, akisisitiza kuwa Muungano ndio msingi wa usalama wa Taifa.

Mwanahabari mkongwe, Balozi Mstaafu John Liundi alishauri kuwa elimu ya Muungano ianze kutolewa tangu ngazi ya shule za msingi ili kujenga uzalendo mapema.