Njombe. Jeshi la Polisi mkoani Njombe linawashikilia Petro Mfugale (35) na Benson Lyambilo (35), wakazi wa Lyamkena mjini Makambako kwa tuhuma za mauaji ya Alfred Mfugale (61).
Watuhumiwa wanadaiwa kumpiga na kitu kizito na chenye ncha kali kichwani na kisogoni hali iliyosababisha avuje damu nyingi hadi kifo chake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amesema hayo leo Desemba 23, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari.
Amesema uchunguzi unaonyesha Alfred aliondoka Novemba 17, 2025 kwenda shambani lakini hakurudi nyumbani hadi mwili wake ulipopatikana Novemba 18, 2025 kilomita chache kutoka shambani kwake.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha alikwenda shambani kwake hakurudi mpaka siku inayofuata mwili wake ulipoonekana kilomita chache kutoka shambani akiwa amefariki dunia,” amesema.
Wakati huohuo, Kamanda Banga amesema Gerod Willa (40), mkazi wa Kijiji cha Madunda anashikiliwa kwa kosa la ubakaji.
Anadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 24, 2025 saa nane mchana.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha mtuhumiwa amekuwa na tabia ya kushinda porini akiwa amejificha na wanapopita wanawake huwafukuzia na kuwabaka.
“Baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa, msako mkali ulianza na kufanikisha kumkamata akiwa amejificha,” amesema.
Vilevile, jeshi hilo linamshikilia mfanyabiashara, Neema Mwalongo (45) akituhumiwa kuuza bidhaa zilizopita muda wa matumizi, zikiwamo pombe kali pakiti 224, soda na vinywaji vingine.
Kamanda Banga amesema upelelezi wa shauri hilo unaendelea kufanyika na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
