Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amesema Muungano wa Tanzania unaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, akionya iwapo vijana hawatapewa elimu sahihi kuhusu misingi ya Muungano huo, upo hatarini kuvunjika.
Hata hivyo, Balozi Christopher Liundi amesema mazungumzo ya wazi na ya mara kwa mara ni njia bora na ya kudumu ya kupunguza chuki na kukabiliana na migogoro ndani ya jamii na Taifa kwa jumla.
Haya yamesemwa leo jijini Dar es Salaam wakati wa semina iliyotolewa na Wizara ya Muungano kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari, iliyobeba mada isemayo: “Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kulinda na Kuendeleza Muungano.’” Akizungumza katika semina hiyo akimuwakilisha mgeni rasmi, Makamu wa Rais, Dk Emmnauel Nchimbi, Waziri Masauni amesema Watanzania wengi hususan vijana ambao wamezaliwa baada ya Muungano, wana mitazamo potofu.
Amesema si kwamba wanafanya makusudi, bali wengi wao hawaelewi historia njema ya Muungano, hali inayochochea mgawanyiko usio na msingi nchini.
Hata hivyo, ametoa rai kwa wahariri wa vyombo vya habari kufanya mijadala mbalimbali inayohusu Muungano itakayowashirikisha vijana kwa kiwango kikubwa chenye lengo la kuwaelimisha.
“Tunakoelekea, vijana hawa tusipowaeleza ukweli watatuzidi kimo. Imefikia mahala tunagawanywa kwa vitu, wale wamepata hiki, wale kile. Wanashindwa kuelewa kuwa hatukuungana kwa vitu; Mzanzibari au Mtanzania Bara akipata fursa, tatizo liko wapi?” amesema Masauni.
Amesema Muungano umeendelea kuwa nguzo ya amani, mshikamano na utulivu wa Taifa, licha ya kuwepo kwa baadhi ya watu wanaoubeza bila kuelewa madhara ya kufanya hivyo.
“Kuna nchi zilikuwa kwenye muungano lakini baada ya kuvunjika, zilitumbukia kwenye machafuko. Mifano ipo hapa Afrika, ikiwamo Sudan na Sudan Kusini; walikuwa na amani lakini baada ya kutengana mambo yalibadilika,”amesema waziri huyo.
Waziri Masauni alisema endapo Muungano wa Tanzania utavunjika, madhara yake yatakuwa makubwa na ya kudumu.
“Dhambi hiyo haitaisha. Watanzania wataanza kugawanyika vipande vipande na heshima ya Taifa iliyojengwa kwa muda mrefu itatoweka,” amesema.
Akitaja matukio ya hivi karibuni ya ubaguzi wa kidini na kijamii yanayojitokeza kwenye mitandao ya kijamii, Masauni amesema ni dalili hatarishi zinazopaswa kukemewa mapema.
“Mliona kuliibuka kauli za ubaguzi na udini; si jambo jema. Tusipende kumung’unya maneno katika mambo ya msingi,” amesema.
Waziri huyo amesema mijadala na uhuru wa kujadiliana ni miongoni mwa hoja zinazojadiliwa kwa kina kwa sasa, akisisitiza Serikali inaliona na kulitambua suala hilo.
“Mijadala na uhuru wa kujadiliana ni hoja ambayo imekuwa ikizungumzwa zaidi. Tutafanyia kazi mambo haya kwa haraka ili watu waweze kuzungumza,” amesema.
Kwa upande wake Balozi Liundi, ni muhimu watu wakakubali kukaa na kuzungumza wanapokosana, kwa sababu kupitia mabishano na majadiliano ya kina, hufikiwa muafaka baada ya mmoja kukubali kuchutama.
“Inaweza kuchukua muda na kuwa na mzunguko mkubwa wa hoja, lakini hufika wakati mmoja anakubali kujifunza na hapo ndipo suluhu hupatikana,” amesema Balozi Liundi.
Amesema Taifa linapaswa kujengwa na kuimarisha mfumo wa mazungumzo kama tiba ya kudumu ya migogoro, akipendekeza kuandaliwa kwa vikao na semina zitakazosaidia kudumisha haki, amani na Muungano.
Tishio la mitandao ya kijamii
Masauni amesema kuwa, kasi ya matumizi ya mitandao ya kijamii imekuwa changamoto katika udhibiti wa maudhui, hivyo kuwataka wahariri kutumia nafasi yao kulinda Muungano.
“Lazima kuwepo habari njema zaidi. Wahariri mpo kwenye muhimili wa nne usio rasmi; mna uwezo wa kujenga au kubomoa Taifa. Epukeni habari za uchochezi,”amesema.
Amesema kuna nchi, vyombo vya habari vimechangia kuchochea migogoro iliyogharimu maisha ya wananchi, hivyo semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo wahariri kufikisha elimu sahihi kwa umma.
Mwanadiplomasia Mwandamizi, Omar Kashera Mjenga amewataka wahariri hao kuwa chimbuko la hoja na mijadala mipana kuhusu umuhimu wa kulinda amani na masilahi ya Taifa, hasa ya jamii inapotofautiana kimtazamo.
Mjenga amewataka wahariri kutokuwa waoga katika kusimamia ukweli na masilahi ya Taifa huku akiwataka wavuke mipaka ya woga na masilahi binafsi wanapotekeleza majukumu yao ya kihabari.
“Wahariri wa habari msijishushe wala kujifungia nyumbani. Vukeni mipaka, lakini mtambue kuwa umoja wetu ndiyo fahari yetu. Kila unachoandika kinapaswa kupimwa kwa kuangalia athari zake kwa Taifa,” amesema Mjenga.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Mstaafu, Salvatory Rweyemamu amewataka wahariri na wadau wengine wa habari kupunguza ushabiki katika uandishi wa habari zinazohusu Muungano wa Tanzania, akisema Muungano ulianzishwa na wazalendo kwa misingi ya ukweli na masilahi ya Taifa.
“Tuwe waangalifu na tuache ushabiki. Ukivunjika hakuna faida yoyote tunayoweza kupata. Tupunguze ushabiki hauna faida; tuandike Muungano kwa kuongozwa na kuzingatia ukweli,” amesema Rweyemamu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Dk Abdallah Mkumbukwa amesema Muungano wa Tanzania una upekee wa kipekee duniani kwa kuwa uliunganisha mataifa mawili yaliyokuwa huru Tanganyika na Zanzibar na umeendelea kudumu kwa zaidi ya miaka 60.
Amesema miungano mingi imedumu kwa muda mfupi kutokana na malalamiko ya upande mmoja kudai kutotendewa haki.
Akitolea mfano Rwanda na Burundi ambazo awali zilikuwa nchi moja chini ya utawala mmoja, lakini baadaye zilitengana na hadi leo zinakumbwa na migogoro ya mipaka.
“Sudani na Sudani Kusini walikuwa kitu kimoja lakini walitengana; pia Umoja wa Afrika Mashariki wa awali uliowahusisha Tanzania, Kenya na Uganda ulivunjika muda mfupi baada ya kuanzishwa. Tofauti na hilo, Muungano wa Tanzania umeendelea kudumu, licha ya Bara na Zanzibar kutenganishwa kijiografia na bahari,” amesema.
Lakini amesema upekee wa Muungano wa Tanzania ni muundo wake wa kiutawala unaounda nchi moja yenye Serikali mbili: Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
“Pia kuna Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na Baraza la Wawakilishi Zanzibar lenye jukumu la kutunga sheria kwa masuala ya Zanzibar,” amesema.
