Yanga yamganda Okello, Mujinga | Mwanaspoti

YANGA kuna majina mawili ya viungo washambuliaji wanapambana nayo na mmoja kati ya hao atasaini kukitumikia kikosi hicho kuanzia dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Januari Mosi 2026.

Kama ambavyo Mwanaspoti liliwahi kuandika, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves anataka kuongeza kiungo mshambuliaji yaani namba 10 na hiyo ni baada ya kuona watu alionao hapo hawampi kitu anachotaka.

Kwenye mipango ya mabosi wa Yanga, kuna majina mawili, la kwanza ni kama mabingwa hao wamevamia kwenye hesabu za mtani wake Simba.

Yanga imevamia kwa kiungo fundi Allan Okello ambaye anaitumikia Vipers ya Uganda, lakini kwa sasa yupo na timu ya taifa ya Uganda katika Fainali za AFCON nchini Morocco.

Yanga imemtuma kiungo aliyekuwa akikipiga katika kikosi hicho, Khalid Aucho, kuzungumza na Okello.

Simba iliwahi kumtaka Okello huko nyuma, lakini licha ya kufanya majaribio mawili ya kumsajili, mchakato huo ulikwamia kwa bosi wa juu wa Vipers anayetia ngumu kumwachia.

Taarifa za ndani kutoka Yanga zililiambia gazeti hili: “Tunakwenda naye vizuri, unajua Okello ni mbunifu sana licha ya mwili wake mdogo, kama akipatikana itakuwa hatua nzuri kwenye kikosi chetu.”

Ukimweka kando Okello, jina lingine ambalo Yanga inapambana nalo ni kiungo Mkongomani, Kikwama Mujinga ambaye naye ni nahodha huko anakoitumikia OC Renaissance du Congo ya kwao DR Congo.

Mujinga ni mchezaji muhimu wa kikosi hicho huku ikielezwa ofa iliyowasilishwa hapo na Yanga, inaendelea kupigwa danadana kutokana na kuhitajika kwake kuendelea kuipambania timu hiyo.

Klabu hiyo iliiambia Yanga, itakubali kumuuza Mujinga mwisho wa msimu huu kwa kuwa kama watamtoa sasa, kikosi chao kinaweza kuyumba kwani hivi sasa kipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ya DR Congo Kundi B kati ya timu 15 kikicheza mechi 12.

Hata hivyo, maamuzi hayo ya Renaissance yamekutana na presha ya Mujinga ambaye analazimisha mabosi wake kumalizana na Yanga haraka.

Kama mipango ya Yanga itatimia, basi mmoja kati ya viungo hao atamalizana na klabu hiyo kwenye hesabu za kukiimarisha kikosi chao msimu huu.