Tume huru ya uchaguzi, katiba mpya na uhaba wa rasilimali fedha ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa na baadhi ya vyama vya siasa kama funzo mojawapo walilopata katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti kuhusiana na hilo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu wamesema kukosekana kwa rasilimali fedha kumeongeza nafasi ya kushindwa kwao.
“Mojawapo ya mambo tuliyojifunza ni kuwa na netwok ya chama, sababu tulikuwa tukifanya mikutano isiyo na mpangilio maalum wa maandalizi ya eneo husika. Pili vitendea kazi, vipeperushi vinavyomwonesha mgombea. Lakini kikubwa ni fedha za kutosha kwa ajili ya uchaguzi, hasa ukilinganisha huwi mgombea peke yako na kwa siku unaweza ukahutubia mikutano tisa,” anasema Doyo Hassan Doyo.
Doyo ambaye aligombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD) anasema chama chao kwa sasa wamejipa likizo ya miezi mitatu hadi mwezi Januari, 2026 wataitisha kikao cha Kamati Kuu ambacho pamoja na mambo mengine, kitafanya tathmini na kueleza mwelekeo wao.
“Sisi baada ya kutoka kwenye uchaguzi tumepumzika kusubiri upepo, sababu vikao vinahitaji pesa na huwezi kumwambia mwanachama kujitolea kuja kwenye kikao cha Halmashauri Kuu au Kamati Kuu, hivyo tunadhani Januari mwishoni tutakuwa na kikao cha Kamati Kuu na baada ya hapo tutakuwa na majibu sahihi ya kukujibu tumejipangaje kwa mwaka 2026,” anasema Doyo.
Naye Katibu Mkuu wa The Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi), Husna Abdallah Mohammed, anasema kwa kupitia katiba ya sasa mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 hakukuwa wa kidemokrasia na hivyo mpango wao kwa mwaka ujao ni kuhakikisha wanasukuma agenda ya Katiba mpya pamoja na Tume huru ya uchaguzi.
“Tume Huru iliyopo ipo kwa jina tu, lakini katika utekelezaji haupo. Kama Mwenyekiti wa Tume anateuliwa na mmoja kati ya wagombea wa nafasi ya urais, huwezi kusema hiyo Tume ni Huru, Tume Huru inapaswa ijisimamie yenyewe isiwe chini ya kiongozi wa chama cha siasa,” anasema Husna Mohammed.
Mtendaji mkuu huyo wa CUF anasisitiza msimamo wa chama chao wa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyotangazwa kwa madai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro mbalimbali ikiwamo waandamanaji kukimbia na masunduku ya kura.
Aidha Katibu Mkuu huyo wa CUF ameibua hoja kwamba kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 watawala hawajawa tayari kupokea mabadiliko yanayotokana na mchakato wa kidemokrasia, jambo lililosababisha kupokwa ushindi katika majimbo kadhaa yakiwamo Nanyamba mkoani Mtwara, Kaliua, Tabora na Mbagala jijini Dar es Salaam.
“Tumejifunza kwamba, watawala bado hawajawa tayari kwa ajili ya demokrasia wako tayari kufanya jambo lolote ili wabaki madarakani, ndio maana utaona kuna baadhi ya majimbo tulishinda lakini wagombea wetu hawakutangazwa,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa African Democratic Alliance (Ada-Tadea), Juma Ali Khatibu anasema baada ya kushindwa kupata kiti hata kimoja cha ubunge, mapema 2026 wamepanga kuanza upya kufanya siasa kwa kuwa karibu na kada ya vijana.
“Tuna mpango wa kuwa karibu na vijana kwa kuwapa semina mbalimbali zinazohusiana na elimu ya uraia na kufahamu umuhimu wa uzalendo, kutunza rasilimali za taifa na hivyo kuwaepusha kujiingiza katika mkumbo wa kuvuruga amani kama ilivyotokea Oktoba 29,2025,” anasema Khatibu.
Vilevile mwanasiasa huyo anasema mwaka 2026 ni mwaka wa kuisoma sana ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kubaini maeneo yasiyofanyiwa kazi kama walivyoahidi.
“Sisi vyama visivyo na uwezo tunapaswa kuisoma ilani ya CCM ili kujua maeneo ambayo wameshindwa kuyafanyia kazi ili tukae upande wa wananchi kuanza kuyapigia kelele yatekelezwe,” anasema.
Khatibu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa nchini, anasema kama chama cha siasa hawana budi kuwa na rasilimali fedha zitakazosaidia kuandaa mikutano mingi ya kampeni pamoja na kuwalipa mawakala watakaozilinda kura.
Kwa upande wake Dk Avelyn Munis, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, ameliambia Mwananchi kwamba, toka kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 bado hawajakaa kikao, na hivyo asingeweza kutoa maelezo binafsi.
“Bado hatujakaa kikao kama chama kutengeneza dira yetu, tutakapokaa Halmashauri Kuu, Kamati Kuu maamuzi yatakayotolewa na maazimio basi yatakuwa na dira yetu ya kuelekea mwaka 2026,” anasema.
Aidha Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema kimejiandaa kuingia mwaka 2026 kwa kuhakikisha wanasukuma agenda ya Tume Huru ya uchaguzi inayokubalika na kuaminika na wananchi.
Akizungumza na Mwananchi Mwenyekiti wa ADC, Shaban Itutu anasema tayari wamekaa kama chama na kufanya tathmini ya mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 na kutoka na azimio la kuingia mwaka 2026 wakiwa na agenda hiyo pamoja na ile ya kuungana.
“Ni kuhakikisha tunakwenda kwenye uchaguzi na Tume inayoaminika na wananchi kwasababu kwa sasa naona kama wananchi wana mashaka na Tume hii. Jambo jingine maoni ya wananchi juu ya uwepo wa katiba mpya na kutazamwa upya kwa matukio ya utekaji hapa nchini, kwamba watekaji wajulikane na wachukuliwe hatua ni mambo yanayochochea hasira na ghadhabu,” anasisitiza.
Katika kuhakikisha mkakati wao wa kuongeza idadi ya wanachama, Mwenyekiti huyo wa ADC anasema mapema 2026 watazindua mtambo wa kielektroniki wa usajili wa wanachama nchi nzima.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo, Isihaka Mchinjita akizungumzia hilo, amesema kuna haja ya kuingia kwenye chaguzi zijazo kukiwa na mifumo thabiti ya uwajibikaji.
“Sisi tunaona kwamba, masuala ya katiba mpya itakayojenga mifumo thabiti ya uwajibikaji na kuweka misingi ya utawala bora sambamba na kunusuru yale yaliyotokea Oktoba 29, 2025 ambayo yalikuwa ni jaribio la kuua demokrasia kwa kuruhusu matumizi makubwa ya nguvu,” alisema.
Mchinjita ambaye alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Lindi Mjini mkoani Lindi, anasema mwaka 2026 lazima uwe mwaka utakaozingatia mifumo imara ya kiuchaguzi na kuleta tafsiri sahihi ya maana ya uchaguzi ni lazima ukuu wa watu wenye kufanya maamuzi uonekane.
Mwenyekiti wa Alliance for African Farmers Party (AAFP), Soud Said Soud anasema wanaingia 2026 huku wakitarajia mabadiliko makubwa yatakayotokana na uundwaji wa katiba mpya ambayo itaruhusu ugawanaji wa madaraka.
“Kuwapo kwa katiba mpya kutapatikana uwigo mpana wa uongozi maana tatizo kubwa Tanzania ni kutokugawana madaraka, madaraka yanang’ang’aniwa na chama kimoja tu. Lakini endapo Tanzania itaweka utaratibu wa kugawana madaraka kama Afrika Kusini, basi nchi itakuwa salama,” anasema.
Soud ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar, amelalamikia ahadi ya serikali kuwapa ruzuku vyama vya siasa kujikimu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wanasema changamoto zinazolalamikiwa na vyama vya siasa zimekuwa zikijirudia kila uchaguzi bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, hali inayodhoofisha imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.
Mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam, Hassan Mohamed, anasema vyama vya siasa vinapaswa kuanza kujipanga mapema zaidi badala ya kusubiri karibu na uchaguzi.
“Tatizo si tume tu au katiba, hata vyama vyenyewe havijiandai. Vinakuja wakati wa kampeni tu, halafu vikishindwa vinadai hawakuwa na fedha au mazingira hayakuwa sawa. Sisi wananchi tunataka kuona vyama vinatufikia hata nje ya uchaguzi,” anasema.
Kwa upande wake Neema John, mfanyabiashara mdogo wa Kariakoo, anasema uchaguzi wa 2025 umewaacha wananchi wengi wakiwa na maswali kuliko majibu.
“Kulikuwa na vurugu, watu walikimbia, wengine walikamatwa. Mpaka leo hatujaelewa kilichotokea. Kama 2026 hawatabadilisha mfumo, wananchi watazidi kukata tamaa kushiriki siasa,” anasema.
Naye Said Msimbe, mkulima wa Kilosa mkoani Morogoro, anasema vyama vya upinzani vinapaswa kuungana badala ya kugawanyika.
“Kila chama kinakuja kivyake, vinapoteza kura. Kama kweli wanataka mabadiliko, waweke maslahi ya wananchi mbele, waungane,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi, mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala, Dk Azikiwe Boraufe anasema kauli za vyama vya siasa baada ya uchaguzi wa 2025 zinaonesha wazi kuwa mzunguko wa uchaguzi nchini bado unaendeshwa bila marekebisho ya kimuundo.
“Unapofika mahali vyama vyote vinakubaliana kuhusu tume, katiba na fedha, maana yake tatizo ni la mfumo, si chama kimoja. Bila mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi, 2026 itakuwa ni mwendelezo wa 2025,” anasema.
Dk Boraufe anaongeza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kutumia kipindi cha baada ya uchaguzi kujenga mifumo ya ndani badala ya kusubiri msimu wa kampeni.
“Huu ndio wakati wa kujenga chama, si wa kupumzika. Vyama vinavyosema vinapumzika vinajidanganya, kwa sababu uchaguzi unaanza kesho,” anasisitiza.
Kwa upande wake mchambuzi mwingine wa siasa, Maulid Maulid, anasema hoja ya ukosefu wa rasilimali fedha ni kikwazo kikubwa lakini si sababu ya msingi pekee ya kushindwa kwa vyama.
“Fedha ni muhimu, lakini hata kama ungekuwa na fedha nyingi bila kuwa na ajenda inayoeleweka kwa wananchi, hushindi. Vyama vinahitaji sera mbadala, si lawama pekee,” anasema.
Anaongeza kuwa 2026 itakuwa mwaka wa kupima kama vyama vya siasa vimejifunza kweli au vinaendelea kuzunguka katika lawama zilezile.
“Ikiwa mjadala utaendelea kuwa tume, katiba na dola bila mikakati mipya ya kisera, basi wananchi wataendelea kuwa watazamaji badala ya washiriki,” anasema.
Kwa ujumla, kauli za vyama vya siasa, wananchi na wachambuzi zinaonesha kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 haukuwa mwisho wa mvutano wa kisiasa bali mwanzo wa mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini, huku macho yakielekezwa mwaka 2026 kama kipindi cha maamuzi mapya au marudio ya historia ileile.
