KONA YA MALOTO: Waraka wa somo la urais kwa wazazi, walimu

Mwalimu shuleni na mzazi nyumbani. Mwambie kijana kuwa haki na wajibu vina uzani sawa. Kama ambavyo mtu anahitaji kutendewa haki, ndivyo ambavyo anatakiwa kutimiza wajibu. Ni maana mbili pacha, sawa na kulwa na doto. Ukisikia kuhusu doto, ujue kulwa yupo.

Ni ukumbusho sawa na wito wa Rais wa 35 wa Marekani, John Kennedy, siku ya uapisho wake kuongoza ofisi namba moja kwenye nchi yake, Januari 20, 1961. Kennedy alisema: “My fellow citizens of the world, ask not what America will do for you, but what together we can do for the freedom of man.” – “Rais wenzangu wa ulimwengu, usiulize nini Marekani itakufanyia, bali nini ambacho kwa pamoja tunaweza kufanya kwa ajili ya ukombozi wa watu.”

Hatari ni kwa taifa, kuwa na kizazi chenye kuamini katika kutengenezewa, badala ya kushiriki kutengeneza.

Hatari zaidi ni kutengeneza jamii za vijana wenye kudhani kwamba wao wapo kupewa haki zao, pasipo kutimiza wajibu. Madhara yake taifa litashamiri jumuiya za walalamikaji.

Mwalimu shuleni, mzazi nyumbani, mwambie kijana asiulize nchi itamfanyia nini, bali yeye kwa nafasi yake ni kipi atafanya kwa kushirikiana na Watanzania wenzake, kuijenga nchi iliyo bora. Taifa la watu milioni 70, ni mzigo kiasi gani, endapo kila mmoja ndani ya nafsi yake, atawaza kufanyiwa bila kuwajibika kuifanya nchi kuwa salama kwa raia wote.

Hili ni somo rahisi la uraia. Mhitimu wa ngazi yoyote ya elimu anapaswa kufaulu. Ina sadifu wimbo wa hamasa nyakati za ujamaa, kwamba “taifa litajengwa na wenye moyo.”

Haikuimbwa kwamba Tanzania ingejengwa na Rais Julius Nyerere, Mwalimu na Baba wa Taifa, bali Watanzania wenye kujituma na wanaojitoa bila kuchoka.

Kijana wa Kitanzania afahamu kwamba Tanzania ni taifa mchanyato. Jamii hadi jamii, kabila kwa makabila. Ni taifa la dini mseto. Kutoka dini moja hadi nyingine, inatakiwa kiwango cha juu cha kuheshimiana na kuvumiliana. Mbele ya nchi, hakuna dini yenye hadhi ya kipeo cha pili na nyingine za kawaida. Kila dini ni bora mno kwa waumini wake. Dini kuwa bora kuliko dini nyingine, hapo huzaliwa janga.

Jamii zote ni sawa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakuna kabila lenye hadhi daraja la kwanza wala la pili. Tanzania haina jamii za watawala na watawaliwa.

Haina jumuiya za matajiri na makabwela, mithili ya Kuomintang na Communist, zilivyojenga matabaka China zamani. Tanzania, yeyote anaweza kuwa yeyote. Kijana aambiwe hivyo, atambue. Vinginevyo chuki inaweza kumhadaa na itamteka.

Simulizi ya Said Salim Bakhresa kuwa alianza kama mshona viatu, kisha mfanyabiashara mdogo, akapanda madaraja hadi kuwa bilionea anayetazamwa leo, hiyo ni kweli.

Kijana afahamu kuwa hadithi ya mbuyu kuanza kama mchicha, humaanisha kila kitu mwanzo wake ni mdogo.

Kariakoo, mabilionea wanazaliwa mwaka hadi mwaka, kizazi kwa kizazi.

Mzazi nyumbani, mwalimu shuleni, mwambie kijana na atambue kwamba kila mwenye mafanikio, ndani yake kuna siri iliyofichwa kwenye nidhamu na ushindi dhidi ya shere. Utesi wa vijiweni na mitandaoni kwamba kila aliyetajirika ameiba au ametumia njia batili, hujenga kizazi cha wavivu wenye kukosa uthubutu.

Haiondoi ukweli kuwa ndani ya dunia kuna majambazi, mafisadi, na matapeli. Wapo wauza dawa za kulevya na wanaotumia madaraka yao kujimilikisha mali.

Hayo yote hayatoi msamaha kwa watu kubweteka na kusengenya vijiweni na mitandaoni kuhusu uhalali wa utajiri wa wengine, badala ya kupambana kwenye njia halali ili kuyasaka mafanikio yao.

Tanzania ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Nchi inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jina “Tanzania” ndilo hasa Watanzania wenyewe waliamua kuiita nchi yao. Tanganyika na Zanzibar ni majina ya kurithi kutoka kwa Wakoloni.

Haihitaji kukaa darasani hata mwezi kung’anua fahari ya jina Tanzania. Jina lililoundwa na Watanzania wenyewe.

Ukombozi wa nchi Tanzania ulipatikana awamu mbili. Desemba 9, 1961, Tanganyika na Januari 12, 1964, Zanzibar. Baada ya kuwafukuza Wakoloni, Watanzania walichagua kuunda nchi yao. Aprili 22, 1964, ni siku ambayo hati ya Muungano ilisainiwa. Kisha, Aprili 26, 1964, tamko la Muungano likatolewa rasmi. Nchi ikawa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Halafu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mzazi nyumbani, mwalimu darasani, mwambie kijana kwamba nchi ilishakombolewa. Wakoloni walifukuzwa. Na uhuru wa Tanzania haufanani na wa Afrika Kusini, Mei 31, 1910.

Makaburu (raia weupe), wakarithi tabia za kikoloni kuwatawala raia weusi kimabavu na kuwanyima haki zote kimsingi.

 Uhuru wa Afrika Kusini ulikuwa sawa na Marekani Julai 4, 1976, Wazungu wakajikabidhi uhuru na kuwafanya weusi kuwa watumwa.

Tanzania ilipopata uhuru, nchi ikawa ya Watanzania wote. Siasa huleta ushindani. Demokrasia ya vyama vingi.

Kijana anapaswa kutambua wanasiasa hutumia njia mbalimbali kutafuta uungwaji mkono. Wapo huzungumza lugha ya ukombozi, utadhani nchi bado ipo kwa wakoloni.

Mwaka 2015, Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, alikerwa na maneno hayo, akasema wanaonadi ukombozi ndani ya Tanzania huru ni malofa!

Kijana anapaswa kuwa na ujazo mzuri wa akili, aweze kutambua lugha za wanasiasa. Hakuna kitu kinachoitwa ukombozi kwenye nchi huru, isiyo na matabaka.

Tanzania ya sasa, ushindani uliopo ni wa kushika dola. Atoke Mtanzania mmoja, ashike mwingine. Watanzania hawa washinde mamlaka, wengine wakose. Ni mchuano wa Watanzania kwa Watanzania.

Ni zama za ushindani wa sera, itikadi, maono na vipaumbele kuhusu kesho ya Tanzania. Uchaguzi hukutanisha Watanzania wanaojali kesho ya nchi.

Kijana ajenge picha katika muktadha huo. Asiingie mkenge wa chuki, kudhani wapo wanaoipenda Tanzania na wengine wanaichukia. Kijana asiachwe bila kuambiwa kwamba mwanasiasa akiona kugawanya watu kunampa faida, atawagawa. Ni siasa na wanasiasa.

Katika uchambuzi wa mwisho, kijana anatakiwa kutambua kuwa hatima ya nchi ipo mikononi mwake.

Kuijenga au kuibomoa. Kuistawisha au kuidumaza.

Taifa litajengwa na wenye moyo. Aliye shuleni asome kwa bidii. Mwenye wito wa kuongoza ajitokeze, aombe ridhaa.

Mfanyakazi atimize wajibu wake, mkulima, mfanyabiashara kadhalika. Kodi zilipwe, nchi isonge mbele.

Kiapo cha juu kiwe kuikabidhi nchi iliyo bora kwa kizazi kinachofuata, kuliko ile aliyoipokea.

Huu ndiyo msingi kuwa Tanzania ya sasa imepiga hatua kubwa kuliko ya Mwalimu Nyerere.

Rais mpaka Rais, Ali Hassan Mwinyi, Mkapa, Jakaya Kikwete, Dk John Magufuli hadi Rais wa sasa, Dk Samia Suluhu Hassan, ni sababu Tanzania kuwa ilivyo sasa.

Kutoka vijiji vya jamii za makabila hadi miji mikubwa na majiji, wilaya zote zinaunganika kwa lami, treni za umeme, ndege zinatua mikoa yote, Tanzania yenye umeme hadi inauza nje ya nchi.

Kijana atambue kuwa Tanzania inaendelea kujengwa.

Na kazi kubwa imefanyika kuifikisha nchi ilipo sasa.