Busara na nasaha za Fyatu kwa mafyatu

Katika kufunga mwaka, nalete somo la kifyatu si kwa mafyatu tu hata kwa wafyatuao mafyatu wasiofyatuka wakafyatua wawafyatuao.

Hili ni somo rahisi lakini gumu lihitajilo ufyatu wa kiwango cha juu. Tuanze kujihoji na kuwahoji wengine. Nani aweza kuleta amani au haki kupitia dhuluma? Amani haiwezi kukaa sehemu moja na shari wala mwanga na kiza.

Adhaniaye anaweza kuviweka viwili hivi pamoja, anajidanganya na kudaganya wengine. Mwanga na kiza ni maadui sawa na upendo na chuki. Hata upendo upende vipi chuki, chuki haiwezi kuupenda au kuzaa upendo bali chuki.

Japo hakuna uongo mzuri, kujidanganya ukadhani umewadanganya wengine ni hatari hata kuliko kudanganywa maana, waweza kushuku au kushukiwa ukaelewa ila siyo kujishuku.

Mzee asiye na busara ni hatari kuliko mtoto mpumbavu kwani hana muda wa kujifunza ikilinganishwa na mtoto mwenye muda wa kuishi na kujifunza. Heri kisu butu kisichoshika kutu kuliko kikali kimalizwacho na kutu.

Uzee unapogeuka au kugeuzwa uzezeta na uchumia tumbo, heri kufa mapema kuliko kuzeeka na kuishia kuwa hovyo kiasi hiki. Mvi ni alama ya hekima. Ijapokuwa, wapo wengi walio nazo ila hovyo kiasi cha kutamani zingeota kwenye mwembe lau watoto hata ndege wale wapate hekima.

Hebu tujifunze zaidi. Uongo na ukweli haviwezi kutangamana wala kuvumiliana. Ukweli ni ukweli na huweka huru wakati uongo ni uongo na humfanya auaminiaye mtumwa hata asifiwe au kujisifu vipi.

Nani aliweza kulaza ubunifu na ubabaishaji kitanda kimoja? Ukifanikiwa, kitanda hata nyumba vitavunjwa vipande tokana na uadui wake.

Sijawahi kudhani wala kushuhudia kujiamini na woga vikiishi pamoja na kupendana achia mbali kuwezekana.

Ajiaminiye kuwa anaweza kuweka viwili hivi pamoja, siyo anajidanganya tu bali anajiaibisha na kuonyesha asiyo na akili wala busara. Nani aweza kuweka imani na shiriki pamoja kama ilivyo imani na uhalisia? Chanya na hasi havitafanana hata vifananishwe vipi. Uchafu ni uchafu hata utukuzwe vipi bado ni uchafu.

Kwanini mja akifa hupelekwa mochwari kabla ya kuzikwa? Simpo. Uzima na ufu haviwezi kuwa sehemu moja kwa wakati mmoja. Kimoja kikiwapo, kingine hutoweka.

Japo siku hizi, wapo wanaohalalisha haramu na kuharamisha halali, ukweli ni kwamba halali na haramu havijawahi kuwa mapacha wala marafiki. Utuli na uoza haviwezi kuwa washirika.

Kadhalika, mwelevu na mjinga hawawezi kukubaliana wala kushindana. Ajuacho mjinga ni ujinga na mwelevu avijua vyote viwili. Heri uwe mwelevu ajifanyaye mjinga kuliko mjinga, tena juha, ajifanyaye mwelevu.

Je, kuna ulevi mzuri wenye siha uwe wa urahibu au maulaji? Ulevi ni ulevi hata uitwe starehe. Ushuzi ni ushuzi hata uwe wa mfalme. Nani mpumbavu awezaye kuuachia mbele ya kadamnasi akajifisifia kafanya jambo jema?

Je, hawapo wachafuao hewa kwa vinywa vyao tena usiowategemea?

            Kuna wakubwa walio wadogo kuliko wadogo walio wakubwa. Heri kuwa mdogo asiyependa ukubwa kuliko kuwa mkubwa mwenye uwezo mdogo katika kuutumia ukubwa. Tembo ana mwili mkubwa ila ana hasira kidogo. Vipi kuhusu nyuki? Nyuki na kijimwili chake kidogo, ana wingi wa hasira.

            Kuna waja wenye macho lakini vipofu na vipofu wanaoona mbali kuliko wenye macho? Hebu fikiria juu ya hili. Ukahaba si wa ngono bali hata wa siasa ni ukahaba. Kuna ulimwengu ambapo mizoga i hai na walio hai waweza kuwa mizoga hata wasichekane.

            Ubinafsi na ulafi ni ugonjwa wa vichaa. Kuna faida na mantiki gani kwa mja kujilimbikizia mali tena kwa kuwaibia na kuwaumiza wenzake ilhali aliikuta na ataiacha?

Ni mwenye akili na busara gani aweza kuonea uchoyo kwa kile ambacho hawezi kukila au kukitumia na kimaliza? Najua hili halipendezi kusema. Ila kwa wenye akili ni shairi au wimbo mtamu. Apandeaye atashuka, na ajikwezaye atashushwa. Hivi mja ni nini hadi ajikweze huku akiwatweza wenzake?

            Je, wajua kuwa mja afarikipo huoza haraka kuliko viumbe wote isipokuwa minyoo na samaki? Kati ya kuku ambaye huungwa auawapo na kuliwa na binadamu ambaye huvishwa na kutupwa nani bora? Ni kipi bora kati ya maguvu na akili? Si kila kitu kinahitaji maguvu japo vyote uhitaji akili.

Hujasikia wahenga wakiasa kuwa akili ni mali? Je, maguvu nayo ni nini? Moto waweza kuchemsha maji hadi yakayeyuka na kukauka. Je, maji hayazimi moto ukapotea? Umdhaniaye yu dhaifu aweza kuwa bora kuliko umdhaniaye kuwa mwenye nguvu. Heri mwenye njaa ya tumbo kuliko ya Kichwa. Heri aliyejishusha kuliko atakayeshushwa.            

Amuoneaye, kumdhulumu au kumuua yule ambaye asiyeweza kumuumba isipokuwa kumdhulumu, hujidhulumu, hujionea, na kujiua asijue japo hawafi siku na kwa namna moja.

Kesho ni bora kuliko jana japo jana ndiyo iizayo kesho kama ambavyo kesho nayo kuna siku itakuwa jana. Heri ya mwaka mpya.