Aliyeshtakiwa kwa mauaji aachiwa huru

Arusha. Mahakama Kuu ya Zanzibar imemuachia huru, Juma Suleiman Juma, aliyekuwa ameshtakiwa kwa kosa la mauaji ya mtuhumiwa wa kosa la wizi, Abdalla Haji Hamdu baada ya Mahakama kujiridhisha hana kesi ya kujibu.

Ilidaiwa mahakamani hapo Septemba 30,2024 katika eneo la Masingini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Juma na wenzake saba (siyo washtakiwa katika kesi hiyo), walimshambulia Abdalla kwa kumpiga na fimbo, kumvalisha tairi la gari, kummwagia petroli na kumchoma.

Ilidaiwa kuwa Abdalla aliwahishwa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Dar es Salaam), ambapo kutokana na majeraha makubwa aliyopata alifariki dunia Oktoba 5, 2024.

Hukumu hiyo ilitolewa Desemba 18, 2025 na Jaji Haji Suleiman Khamis, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya jinai namba 48/2024, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanywa Oktoba 7,2024 na kubaini kuwa marehemu alikuwa na majeraha makubwa ya moto yaliyofunika mwili kwa zaidi ya asilimia 80.

Kwa mujibu wa nakala hiyo ya hukumu, upande wa mashtaka ulieleza Mahakama kuwa utakuwa na mashahidi 12 na vielelezo saba ila wakati wa usikilizwaji uliita mashahidi wanne pekee.

Shahidi wa kwanza ni Haji Hamdu Ali (baba wa marehemu), Sada Abdulrahman Saleh (dada wa marehemu), Maryam Mussa Masoud  (jirani wa marehemu) na mpelelezi wa kesi hiyo, F.6170 Sajenti Hassan Kassim Mohamed.

Kumbukumbu za Mahakama zinaonyesha kuwa hakukuwa na vielelezo vilivyotolewa wakati wa kesi hiyo ikiwa ni pamoja na ushahidi muhimu kama vile ripoti ya kifo, picha ya eneo la tukio au ushahidi wowote wa kimatibabu.

Baada ya Mahakama hiyo kusikiliza kesi ya upande wa mashtaka, chini ya kifungu cha 263 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai 2018, ilikuwa na wajibu wa kuangalia iwapo ushahidi huo unafanya mshtakiwa awe na kesi ya kujibu au la, ambapo baada ya kupitia ushahidi huo ilibaini mshtakiwa hana kesi ya kujibu.

“Baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka, imebainika kuwa hakuna shahidi hata mmoja aliyemuona mshtakiwa akitenda kosa hilo au kushiriki shambulio dhidi ya marehemu.

“Zaidi ya hayo hakuna ushahidi wa kimatibabu uliowasilishwa mbele ya mahakama, ripoti baada ya kifo ambayo ni msingi katika kuthibitisha ukweli wa chanzo cha kifo katika shtaka la mauaji, na zaidi hakuna kumbukumbu au vielelezo vilivyotolewa ikiwemo picha za eneo la tukio,” amesema Jaji.

Jaji huyo amesema kutokuwepo kwa ushahidi wa kimatibabu na wa kiuchunguzi hasa baada ya kifo ni hatari kwa kesi ya upande wa mashtaka.

“Mahakama hii inaona kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuanzisha kesi ya msingi dhidi ya mshtakiwa, ushahidi uliotolewa hata kama utachukuliwa kwa kiwango cha juu zaidi haitoshi mshtakiwa kujitetea,”amesema Jaji na kuongeza

“Mshtakiwa anaonekana hana kesi ya kujibu kwa hiyo ninaamuru aachiliwe huru isipokuwa kama ameshikiliwa kwa sababu nyingine.”