Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewahimiza wakazi kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa busara, huku wakizingatia kuweka akiba kwa ajili ya mahitaji ya Januari, ikiwemo ada za shule.
Kanali Mtambi ametoa wito huo leo Jumatano, Desemba 24, mjini Musoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usalama mkoani humo kuelekea sikukuu hizo.
Amesisitiza kuwa pamoja na kusherehekea, wakazi wanapaswa kukumbuka majukumu na mahitaji ya baada ya sikukuu, akieleza kuwa maisha yanaendelea na sikukuu zisije zikawa kikwazo cha utekelezaji wa mambo ya msingi.
“Tule ‘bata’ lakini tukumbuke Januari sio mbali, na Januari ina majukumu mengi likiwamo la watoto kwenda shule kwa hiyo wakati tunaburudika tukumbuke tuna majukumu makubwa mbele yetu,” amesema.
Kuhusu hali ya usalama mkoani humo, Kanali Mtambi amesema ni shwari na amewahakikishia wananchi kuwa wanaweza kusherehekea sikukuu hizo kwa amani bila hofu.
Akiwataka kila mmoja kuwa mlinzi wa amani, akisisitiza jukumu la kulinda usalama ni la kila Mtanzania.
Ameongeza kuwa usalama barabarani ni miongoni mwa vipaumbele vya vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo, akibainisha kuwa uzoefu unaonesha ajali huongezeka nyakati za sikukuu.
“Kuna mtu anaendesha gari mwendo kasi ajabu yaani anapita kama mshale sasa vitu kama hivi hatutaviruhusu, kwani vimekuwa vikisababisha majeruhi au vifo bila sababu ya msingi mambo kama haya hatuyataki,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wameunga mkono kauli ya Mtambi, wakisema jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya mahitaji mengine ya msingi baada ya sikukuu.
“Kwenye mitandao ya kijamii mara nyingi tumekuwa tukiona namna watu wanavyozungumzia suala la ada, japokuwa wanafanya utani lakini ule ndio uhalisia yaani tunajisahau sana tunakuwa kama hatujui kuwa kuna watoto kwenda shule tunapaswa kubadilika, tufurahi lakini tukumbuke kuna Januari,” amesema Emmanuel Gabo.
Amina Ibrahim amesema jamii inapaswa kufahamu kuwa sherehe za mwisho wa mwaka si mwisho wa maisha, hivyo kuweka akiba kwa ajili ya matumizi mengine ya baadaye ni jambo muhimu na linalopaswa kupewa kipaumbele.