Dar es Salaam. Mbunge wa Bunda Mjini (CCM), Ester Bulaya amesema kuwawezesha na kuwasaidia wananchi wa jimbo hilo, wakiwemo wanaoishi katika mazingira magumu ni miongoni mwa vipaumbele vyake vikuu.
Kwa kuanzia Bulaya ametoa msaada wa vyakula kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwenye kituo cha Kuzungu, Magereza ya Wilaya ya Bunda, na kutunisha mfuko wa bodaboda.
Bulaya ametoa msaada huo kwa nyakati tofauti jana Desemba 23,2025 ikiwa ni kuwatakia heri ya sikukuu ya Krismasi itakayoadhimishwa kesho Alhamisi Desemba 25.
“Tumewapa bidhaa mbalimbali, ikiwemo sukari, sabuni, maharagwe, mafuta ya kupikia, lakini pia kwa wasichana tumetoa taulo za kike. Licha ya kuwa ni jukumu langu kama mbunge, lakini pia mimi ni mama.”
“Lakini kuna maeneo mengine yanahitaji wa msaada, tukiwa kama viongozi na mwakilishi ni jukumu letu kutoa mkono wa heri wa sikukuu,” amesema Bulaya.
Sambamba na hilo, Bulaya amesema amekutana na umoja wa wasafirishaji Bunda na kuwapa Sh1 milioni ili kutunisha mfuko wa kukopeshana.
“Hii ni desturi yangu, nafanya kwa fedha zangu na ndio nimeanza. Lakini kuna vingine tunavipigania serikalini vitakuja, kwa sababu mwisho wa siku nahitaji kuacha alama mimi na Rais Samia Samia Suluhu Hassan na CCM.”
Msimamizi wa kituo hicho, Mtawa Arta Lleshaj amemshukuru Bulaya kwa kujali ustawi wa jamii na kuendelea kuwa karibu na wananchi wake.
Lleshaji amesisitiza kuwa mchango huo ni ishara ya uongozi wenye huruma na kujitoa kwa dhati, na akaomba Mungu aendelee kumbariki Bulaya katika majukumu yake ya kulitumikia Taifa.
Aidha Bulaya ametoa mahitaji ya sare za shule kwa watoto wanaotoka kaya maskini wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2026 jimboni humo.