DKT. MWIGULU: MTENDAJI MKUU WA TEMESA NA MENEJIMENTI YAKE WAFUTWE KAZI

-Aagiza uchunguzi ufanyike kubaini sababu za uharibifu wa mara kwa mara wa vivuko

WAZIRI MKUU Dkt. Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza kufutwa kazi na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) pamoja na Menejimenti ya wakala huo kutokana na ubadhilifu wa zaidi ya shilingi bilioni 2.5.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kufanya uchunguzi wa vivuko vyote ili kubaini vyanzo vya uharibifu kwa sababu kuna taarifa kwamba vivuko hivyo vinaharibiwa kwa makusudi ili wahusika waweze kujipatia fedha kupitia matengenezo.

Amesema uamuzi huo unatokana na matokeo ya tume maalumu iliyoundwa ndani ya kuchunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma katika wakala huo. “Vyombo husika vichukue hatua kwa wahusika, haya mambo ya kutoheshimu fedha za umma, kutokuwa na huruma na Watanzania lazima yafike mwisho.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatano, Desemba 24, 2025 akizungumza na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na wakazi wa Kigamboni akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji wa huduma katika kivuko cha Magogoni, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

 Amesema ubadhilifu uliofanyika ni sawa na watendaji hao kugawana vivuko pamoja na kuiba nauli zinazotolewa na wananchi mambo ambayo yanamkera Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na amewaagiza wayakomeshe ili wananchi waendelee kupata huduma bora na za uhakika.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega afanye mawasiliano na wizara ya fedha kuhakikisha fedha za malipo ya utengenezaji wa vivuko zinatolewa kwa wakati ili zoezi la ukarabati liweze kukamilika na vivuko hivyo viweze kutoa huduma. Serikali inavivuko vitatu katika eneo la Kivukoni/Kigamboni na kwa sasa kinachonfanyakazi ni kimoja tu.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Moses Mabamba amesema Serikali inamiliki vivuko vitatu kwa ajili ya Kivukoni na Kigamboni ambapo kwa sasa kinachotoa huduma ni kimoja tu cha MV. Kazi huku kivuko cha MV. Magogoni kipo kwenye matengenezo Mombasa tangu 2023.

Amesema matengenezo hayo ambayo yanagharimu takribani shilingi bilioni 7.5 yamefikia asilimia 70 huku kivuko kingine cha MV. Kigamboni kipo katika matengenezo kwenye kampuni ya Songoro Marine, Kigamboni. “…Kabla ya kuharibika kwa vivuko hivyo tulikuwa na uwezo wa kukusanya shilingi milioni 20 kwa siku ila kwa sasa tunakusanya shilingi milioni 3.61 hadi shilingi milioni nne.”

Naye, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Bakhresa Group, ambao wameingia ubia na Serikali kutoa hutua ya vivuko, Hussein Sufian amesema walianza kutoa huduma mwanzoni mwa mwaka huu baada ya vivuko vya Serikali kupata hitilafu na walianza na vivuko vinne na sasa wanavivuko nane ambavyo kila kimoja kinauwezo wa kubeba watu 200.

Amesema awali walikuwa wanasafirisha watu 20,000 kwa siku na sasa wanasafirisha watu 50,000 hadi 100,000, kutokana na wingi wa abiria wanakusudia kuongeza kivuko kingine ili waweze kukidhi mahitaji. Vivuko hivyo vinatumia muda wa dakika tano hadi 10 ikitegemea na hali ya bahari.