Kocha Fountain Gate avamia Championship

FOUNTAIN Gate imeibuka na hesabu tofauti, wakati wengine wakisaka mastaa kutoka Ligi Kuu Bara na nje ya Tanzania, yenyewe imekimbilia Ligi ya Championship kuangalia nyota wa kuimarisha kikosi chao.

Hesabu hizo zimeibuliwa baada ya kocha wa kikosi hicho, Mohammed Ismail ‘Laizer’ kuonekana kwenye mechi mbalimbali za Ligi ya Championship akifuatilia kwa umakini huku akiwa na peni na karatasi.

Laizer alionekana kwenye mechi ya Mbeya Kwanza ikiifunga B19 mabao 5-0, huku akiwa na kazi ya kuandika mambo mbalimbali kwenye karatasi yake, mechi iliyopigwa mkoani Lindi.

Kocha huyo pia akaibukia Transit Camp ilipocheza dhidi ya Barberian ambapo wanajeshi hao walishinda kwa mabao 2-0. Mechi ilichezwa Uwanja wa Kituo Cha Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) uliopo Kigamboni, Dar.

Taarifa kutoka Fountain Gate zililiambia Mwanaspoti, Laizer amekuwa akitafuta wachezaji wenye vipaji vikubwa kwenye ligi hiyo baada ya kupata baraka za uongozi wa juu.

“Ni kweli kocha anatafuta wachezaji wapya lakini tumeona tuanzie Championship na kuna wachezaji wengi bora sana na yeye alikubali ndiyo maana mmemwona huko.

“Bado hajatuletea alichokipata, lakini tukikamilisha mtapata taarifa kupitia kurasa zetu rasmi za klabu tutaweka hadharani kila kitu,” kilisema chanzo hicho.

Desemba 29, 2025, Fountain Gate inatarajiwa kurudi uwanja wa mazoezi kuendelea na maandalizi ya mechi zijazo za Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Kikosi hicho kilikwenda mapumziko kikiwa kimecheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara msimu huu, kikishinda tatu, sare moja na kupoteza sita na kukusanya pointi 10 katika nafasi ya nane.