BAADA ya Mwanaspoti kuripoti beki wa kati wa Mashujaa, Abdulmalik Zakaria yupo mbioni kujiunga na Singida Black Stars, mwenyewe amefichua ni kweli ameshamalizana na maafande wa Mashujaa na kwamba mipango yake ni kumaliza msimu akiwa na chama jipya kabisa.
Zakaria amemalizana na Mashujaa kwa kuwashukuru viongozi, wachezaji wenzake na benchi la ufundi kwa muda waliokuwa pamoja huku akiweka wazi kuwa anaenda kutafuta changamoto nyingine nje ya timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, beki huyo alisema ni mapema kwake kuweka wazi ni timu gani anaenda kucheza licha ya kwamba ni kweli ameshasaini mkataba hivyo wadau na mashabiki zake wasubiri taarifa maalum kutoka kwa klabu atakayocheza.
“Ni kweli nimemalizana na Mashujaa baada ya makubaliano ya pande mbili na tayari nimesaini mkataba na moja ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu na nipo tayari kwa changamoto mpya naheshimu uwezo wa nyo-ta waliopo na najua sio rahisi kushindana nao ila nimejiandaa kuhakikisha napata nafasi ya kucheza,” alisema Zakaria na kuongeza;
“Wao ni bora nami ni bora ndio maana wameniona na kuona umuhimu wa kuniongeza kwenye kikosi chao hakuna timu ambayo haina changamoto ya ushindani wa namba kwani eneo moja linasajiliwa wachezaji zaidi ya wawili aliyebora ndio anaanza.’’
Zakaria alisema ushindani ndio chachu ya kukuza ubora hivyo anapenda ushindani.