TRA yamgeukia beki wa Coastal

KLABU ya TRA United imeanza harakati za kuimarisha kikosi chake katika dirisha dogo la usajili linalota-rajiwa kufunguliwa Januari Mosi 2026 baada ya kuonyesha nia ya kuhitaji huduma ya beki wa kati wa Coastal Union, Haroub Arola.

Taarifa kutoka ndani ya TRA United, zinaeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo una mpango wa kumsajili beki huyo moja kwa moja iwapo makubaliano na Coastal Union yatafikiwa mapema, ili aingie haraka katika mfumo wa timu na kusaidia maboresho yanayohitajika wakati msimu ukiendelea.

Hata hivyo, endapo dili la kumsajili jumla litakwama, TRA United imeweka mezani chaguo la kum-chukua Arola kwa mkopo hadi mwisho wa msimu, ikiwa ni mkakati wa kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi bila kusubiri dirisha kubwa la usajili.

Chanzo cha kuaminika kimeliambia Mwanaspoti kuwa, mazungumzo kati ya pande husika tayari ya-meanza, ingawa bado yapo katika hatua za awali huku kila upande ukijaribu kulinda maslahi yake kabla ya kufikia makubaliano ya mwisho.

Hatua ya TRA United kuingia mapema sokoni kuelekea dirisha dogo inaonesha dhamira ya klabu hiyo kuboresha matokeo katika michezo inayofuata ya ligi, baada ya kubaini upungufu uliopo ndani ya kikosi hicho.

Endapo usajili huo utakamilika, Arola anatajwa kuwa chaguo sahihi la kuongeza ushindani, utulivu na uzoefu katika safu ya ulinzi ya TRA United, hasa katika kipindi hiki ambacho ushindani wa Ligi Kuu umeendelea kushika kasi.