Enock Jiah kambi popote | Mwanaspoti

KIUNGO mshambuliaji Mtanzania aliyekuwa anacheza Ligi Kuu ya Oman katika klabu ya Fanja, Enock Jiah amerejea nchini na kwa sasa anasikilizia klabu za Ligi Kuu Bara itakayomvutia kimasilahi ili ajiunge nayo kwani yeye ni kambi popote.

Jiah alitumikia Fanja kwa msimu mmoja akijiunga nayo mapema mwaka huu akitokea KMKM na kwa sasa yupo huru na menejimenti yake imeweka wazi baadhi ya timu zimemfuata kwa mazungumzo.

Nyota huyo kabla ya kutimkia Uarabuni, amewahi kutamba katika Ligi Kuu na timu za Ihefu, Coastal Un-ion, Mwadui na Mbeya Kwanza, lakini akizitumikia pia Mlale JKT na Mbeya Kwanza katika Ligi ya Cham-pionship.

Akizungumza na Mwanaspoti, Jiah alisema kwa sasa kiu yake ni kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kupata uzoefu wa kutosha Oman, kwani anataka kujifua na kuimarisha kiwango chake ili kurejea nje ya nchi.

“Kwa sasa ni mchezaji huru natamani kucheza hapa nyumbani Tanzania kutokana na ushindani uliopo kwa sasa katika ligi yetu, naamini nitaimarika zaidi na kupata tena timu ya nje,” alisema Jiah, huku msimamizi wa kiungo huyo, Ramadhan Chagula bila kutaja majina na idadi ya timu, alisema tayari zipo zilizobisha hodi na kuanza mazungumzo, huku kipaumbele chao ni kucheza Ligi Kuu Bara.

“Hadi sasa kuna timu tuko katika mazungumzo nazo kama maongezi yatakwenda vizuri kuna moja ya timu anaweza kutumikia msimu huu. Ligi ya Tanzania inabadilika kila muda unavyozidi kwenda kila timu sasa hivi inapambana,” alisema Chagula na kuongeza;

“Lengo kubwa ni kurudi tena nje ya nchi, lakini kwa kipindi hiki ambacho kamaliza mkataba na Fanja tumeona ni vizuri kuendelea na kazi hapa nyumbani wakati ambao tunasubiri ofa za nje ambazo tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya timu pia.”