KOCHA Mkuu wa KMC, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ amesema timu haiwezi kufunga bila ya kuwa na washambuliaji wenye ubora wa kuona lango, hivyo mpango wa kwanza ndani ya timu hiyo ni kufanyia kazi eneo hilo dirisha la usajili sambamba na kumchomoa beki mmoja Zimamoto.
Baresi amejiunga na KMC kuziba pengo la Marcio Maximo aliyefikia makubaliano ya kuvunja mkataba baada ya kuiongoza katika mechi tisa za Ligi Kuu Bara na kushinda moja, sare moja na kupoteza saba, kitu kilichowalazimisha mabosi wa klabu hiyo kuachana naye katikati ya safari.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baresi alisema anaendelea kukaa na timu ili kubaini upungufu lakini kwa muda aliofanya pamoja mazoezi na timu amebaini timu inamapungufu eneo la ushambuliaji tayari uongozi umefanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji ili kuongeza nguvu eneo hilo.
“Huwezi kupata mabao kama hauna washambuliaji bora sina maana KMC haina wachezaji wa aina hiyo wapo tutaendelea kuelekezana zaidi ili kuendana na kasi ya timu pinzani lakini pia tumeingia sokoni kutafuta wengine ambao watakuja kuongeza nguvu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mashujaa, Mlandege na Tanzania Prisons.
“Ukiondoa eneo hilo pia ambalo tayari limeonekana kupwaya kwa namba katika mechi zilizochezwa hadi sasa pia nina mpango wa kusajili beki wa kati ambaye tayari uongozi umeanza mazungumzo naye kutoka Zimamoto ili kuja kuongeza nguvu,” alifafanua Baresi.
Bares alisema anaamini kama ataongeza wachezaji wenye ubora kwenye nafasi hizo atakuwa na kikosi kizuri ambacho kitarudisha morali na ushindani licha ya kuweka wazi kuwa haitakuwa rahisi bila ya kuwa na mikakati imara.
“Dirisha dogo sio la kuimarisha timu ni la kuziba mapengo ambayo yameonekana kutokuwa na tija baada ya usajili mkubwa lakini kwa KMC kuna kazi kubwa ya kufanya kwani changamoto ni nyingi umo-ja na ushirikiano mzuri utakuwa tija ya kujenga timu bora.”
KMC ndio inayoburuza mkia katika Ligi Kuu kwa sasa ikiwa ina pointi nne, ikiwa imefunga mabao mawili tu yote yakifungwa na Daruwesh Saliboko, huku yenyewe ikifungwa 14 kupitia mechi tisa.
