Wawili wakutwa na kesi ya kujibu, wakituhumiwa kusafirisha bangi

Dara es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemkuta na kesi ya kujibu Kulwa Mathias na mwenzake Edina Paul, wanaokabiliwa na shtaka moja la kusafirisha bangi.

Hivyo, washtakiwa hao wanatakiwa kuanza kujitetea Desemba 29, 2025.

Mathias na Edina, wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 512.50.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 11, 2024 eneo la ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, kinyume cha sheria.

Uamuzi huo umetolewa leo, Jumatano Desemba 24, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao wa mashahidi 12 na vielelezo 11.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Adolf Verandumi akishirikiana na Neema Kabodya aliieleza Mahakama hiyo kuwa kesi imeitwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Baada ya shahidi wa 12 kumaliza kutoa ushahidi wake, upande wa Jamhuri ulifunga ushahidi wake na ndipo mahakama ilipopitia ushahidi wa mashahidi hao wa upande wa mashtaka na kuwakuta washtakiwa hao kuwa wana kesi ya kujibu hivyo wanatakiwa waanze kujitetea.

Hata hivyo, washtakiwa hao baada ya kukutwa na kesi ya kujibu, walidai kuwa watajitetea wenyewe kwa njia ya mdomo na hawatakuwa na shahidi  wala kielelezo.

Hakimu Makube baada ya kusikiliza maelezo ya washtakiwa hao, aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 29, 2025 kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 5, 2025 na kusomewa kesi ya jinai namba 5543 ya mwaka 2025.