::::::::
Mazingira bora ya biashara nchini, yakiwemo mifumo rafiki ya kikodi pamoja na urahisi wa utoaji wa mizigo bandarini, yameendelea kuwa chachu kubwa ya kuvutia uwekezaji wa kampuni za kigeni Tanzania, hali inayochochea ukuaji wa sekta ya biashara, ushindani wa soko na upatikanaji wa bidhaa bora kwa watumiaji.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya IBKI Enterprises, Ibrahim Kiongozi, kampuni inayojishughulisha na uuzaji na usambazaji wa bidhaa za Haier nchini Tanzania, wakati wa uzinduzi wa duka la sita la bidhaa za Haier, akieleza kuwa mazingira hayo yameongeza imani ya wawekezaji na kuwezesha upanuzi wa shughuli za kibiashara.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda wa Haier anayesimamia Afrika Mashariki, Liu Chi Leon, amesema kuwa soko la Tanzania lina fursa kubwa ya ukuaji wa biashara za vifaa vya kielektroniki, akibainisha kuwa kuimarika kwa mazingira ya biashara kumeifanya Haier kuongeza uwepo wake nchini, jambo litakaloongeza ushindani wa bidhaa zenye ubora wa kimataifa kwa manufaa ya watumiaji.
Aidha, kampuni ya Haier imetangaza mpango wa kuanzisha viwanda vya kuunganisha vifaa vya kielektroniki hapa nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira kwa vijana, kuimarisha uhamishaji wa teknolojia na kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza viwanda, kuongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha uchumi wa taifa kwa ujumla.




