Neno uzalendo linavyozua mjadala | Mwananchi

Dar es Salaam. Upi uzalendo kati ya kukosoa au kuwa mtii kwa Serikali na mamlaka? Ndilo swali linaloibua mijadala katika mitandao ya kijamii, kila upande ukiona unachokifanya kinaakisi msamiati huo.

Wapo wanaouhusisha uzalendo na matendo ya kuikosoa Serikali wakisisitiza kuwa kukosoa, kuhoji na kusimamia uwajibikaji ni kitendo halisi cha kizalendo.

Lakini, upande mwingine unauona uzalendo ni kulinda mamlaka ya dola, kutopingana na utendaji wa Serikali na kuonyesha utiifu kwa nchi na mamlaka zake.

Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ya Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) Toleo la pili, neno uzalendo limetafsiriwa kuwa, hali ya mtu kuipenda sana nchi yake kiasi cha kuwa tayari kufa kwa ajili ya kuitetea.

Katikati ya mvutano huo na tafsiri ya Kamusi, swali linabaki uzalendo ni nini, unapaswa kufanywa kwa ajili ya nani na mzalendo ni mtu anayeenenda vipi, maswali yanayoangaziwa katika uchambuzi wa kisiasa.

Kukosoa ni uzalendo lakini…

Akijadili suala hilo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku ametoa tafsiri inayolandana nay a kamuzi, akisema uzalendo kuwa mapenzi yasiyo na mipaka kwa nchi na inapolazimika unakwenda kuipigania na kuifia.

“Mapenzi ya nchi yako kwa kila hali na kuipigania na kuwa tayari kuifia, huo ndiyo uzalendo kwa tafsiri ya haraka,” amesema.

Butiku amesema mapenzi hayo hayamaanishi kwamba usikosoe pale panapoonekana haja ya maboresho kuhusu jambo fulani ndani ya nchi unayoipenda.

“Kukosoa kitu si kwamba hukipendi, ni kwamba unataka kiboreshwe, ila inategemea unatumia lugha na matendo gani kufanya ukosoaji,” amesema.

Butiku aliyewahi kuwa msaidizi wa Mwalimu Julius Nyerere, amesema kitu unachokipenda huwezi kukikosoa kwa lugha na matendo yanayokivua nguo, lakini hiyo haimaanishi usikikosoe kinapokosea.

Kuhusu neno uzalendo kuhusishwa na sifa kwa Serikali, amesema ni zaidi ya hapo, mzalendo hutangaza mema na mazuri, kuisifu nchi yake, lakini haiondoi umuhimu wa kusahihisha inapoonekana kuna haja hiyo.

“Pale inapobidi na kutoa kauli ya kusahihisha ni muhimu kukosoa, lakini kwa heshima na nia njema ya kutotaka kubadilisha au kuvua nguo kile unachokipenda,” amesema.

Amesema ndio maana kuna neno la kujisahihisha, mnapoona kuna makosa mahali kama alivyotaka Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake.

Hata hivyo, amesema kukosoa na kusahihisha ni tofauti na kupinga, akifafanua upinzani kwa muktadha wa utawala, ni kupingana ili kumwondoa aliyepo madarakani utawale wewe.

Hoja kama hiyo, imetolewa na Mshauri wa Siasa katika moja ya taasisi za kimataifa, Dk Conchesca Mselem aliyesema katika jamii ya kidemokrasia, kukosoa ni haki ya kikatiba na nyenzo muhimu ya uwajibikaji, hivyo ni uzalendo.

“Kukosoa kwa hoja, kwa nia ya kurekebisha na kuboresha ni uzalendo kwa sababu kunalenga kulinda rasilimali za Taifa, haki za wananchi na mustakabali wa vizazi vijavyo,” amesema.

Lakini kukosoa kwa uongo, matusi, au kuchochea machafuko, amesema kunapoteza uhalali wake na kugeuka kuwa hatari kwa Taifa.

Amesisitiza uzalendo haupimwi kwa ukali wa sauti, bali kwa usahihi wa hoja na usafi wa nia.

Kwa mtazamo wa Dk Mselem, uzalendo unapaswa kufanywa kwa ajili ya Taifa na watu wake. Kwa sababu Serikali hubadilika, viongozi huja na kuondoka, lakini Taifa na wananchi hubaki.

“Uzalendo unaweka mbele ustawi wa watu, elimu bora, afya, haki, ajira, usalama na fursa sawa. Serikali ni msimamizi wa dhamira hiyo, inapofanya vizuri, uzalendo hujitokeza kwa kuunga mkono. Inapokosea, uzalendo hujitokeza kwa kuikosoa ili irekebishe,” amesema Dk Mselem.

Tunachanganya uzalendo na utaifa

Upo mkanganyiko wa tafsiri kati ya neno uzalendo na utaifa, suala ambalo Dk Sabatho Nyamsenda, mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema linawachanganya watu.

Kitaalamu, amesema utaifa ni mpana zaidi na tafsiri yake ni hali ya mtu kuwa mtii kwa Taifa na nchi yake na si watawala wala viongozi waliopo madarakani.

Ameeleza mwenye sifa ya utaifa, mara nyingi utii wake ni kwa nchi yake na si viongozi au chama husika, kwa kuwa hivyo ni vitu vinavyopita.

Katika ufafanuzi huo, amemtaja Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa mfano sahihi wa mtaifa, kwani pamoja na kuiasisi Tanzania, aliikosoa ilipokosea.

“Pamoja na yeye kuunda Serikali ya kwanza zikafuata nyingine, zilipokosea hakuacha kuzikosoa. Kwa ujumla kila alichokifanya kilikuwa kwa ajili ya Taifa na sio watawala wa wakati husika,” amesema.

Ameeleza utaifa ndilo eneo ambalo kundi kubwa la wakosoaji na wanaharakati wanaangukia, ingawa baadhi yao wanajiita wazalendo kimakosa.

Kwa upande wa uzalendo, Dk Nyamsenda amesema mara nyingi ni utii kwa nchi na mamlaka zake. “Kwa hiyo mtu ambaye anatii nchi, alama za Taifa, bendera zake huyo ni mzalendo.”

Ameeleza mara nyingi muhamasishaji wa uzalendo ni mamlaka au Serikali iliyopo madarakani na yenyewe itafundisha nyimbo za nchi, bendera za taifa na kuwafundisha watu kuvitii.

“Kazi ya mtawala ni kuwafanya watu kuwa watiifu kwake na wasifie mamlaka kwa namna zilivyo na wasihoji hata mamlaka zikikosea,” amesema.

Kwa mtazamo wa Dk Nyamsenda, raia yeyote anapaswa kuwa na utaifa badala ya uzalendo, kwa kuwa kufanya hivyo kuna masilahi na kunawajibisha zaidi.

Amesema utaifa sio kuvaa bendera za Taifa pekee, bali ni kuwa na imani na utii wa dhati kwa nchi kwa masilahi ya nchi.

Uzalendo si maneno ni matendo

Kwa mtazamo mwingine, Mchambuzi wa Siasa, Said Majjid amesema uzalendo ni dhana pana inayohusisha mapenzi ya dhati kwa nchi, kuheshimu misingi ya Taifa, kulinda masilahi ya wananchi na kuenzi haki, uhuru na ustawi wa jamii, vitu ambavyo vinatakiwa kuonekana katika matendo.

Amesema uzalendo hauishii kwenye maneno mbele za watu, bali unaonekana kwenye matendo yako. Kwa raia anavyoheshimu sheria na anavyosimamia haki ya mwenzake.

Hata hivyo, amesema uzalendo wa kweli haufungwi kwenye kutoikosoa Serikali kwa hali yoyote, kwani maendeleo kwa sehemu kubwa yamepatikana kwa sababu ya raia waliothubutu kuhoji, kupendekeza na wakati mwingine kupinga sera au uamuzi usiokuwa na manufaa kwa umma.

“Kutofautiana na Serikali si kukosa uzalendo. Hata hivyo, upinzani unaoongozwa na chuki, propaganda au ajenda binafsi nao hauwezi kuitwa uzalendo,” amesema.