Waziri Mavunde alivyobadili maisha ya Scholastica

Dodoma. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitembelea familia ya Scholastica Shitebi, mwenye ulemavu anayeishi mkoani Shinyanga ambaye alikutana naye miaka mitatu iliyopita jijini Dodoma, akiomba msaada wa ada ya mwanawe aliyekuwa na ufaulu mzuri shuleni.

Mavunde alikutana na Scholastica karibu na ofisi yake Dodoma, ambako mwanamke huyo alikuwa akiomba msaada kwa wapita njia ili apate ada ya mwanawe.

Baada ya kusikiliza maelezo yake, waziri huyo alimsaidia mashine ya kushonea (cherehani), akamrudisha Shinyanga na kuanza kugharamia masomo ya mtoto wake.

Mtoto huyo, Gregory Lumwaga kwa sasa yupo kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Don Bosco Didia mkoani Shinyanga.

Kwa mujibu wa Mavunde, juhudi hizo zimezaa matunda baada ya mwanafunzi huyo kuendelea kufanya vizuri kielimu, ambapo hata kwenye mtihani wa majaribio mwaka huu amepata ufaulu wa daraja la kwanza.

Akizungumza leo Jumatano Desemba 24, 2025 wakati wa ziara hiyo, Mavunde amesema aliguswa alipobaini kuwa Scholastica alisafiri zaidi ya kilomita 400 kutoka Shinyanga hadi Dodoma kutafuta ada ya mtoto wake.

Amesema tukio hilo lilimpa hamasa ya kumsaidia, hasa baada ya kuona bidii na matokeo mazuri ya mwanafunzi huyo.

“Nilikutana na mama yake Dodoma karibu na ofisi yangu. Aliniambia amefika kutafuta msaada wa kumwezesha mwanawe kuendelea na masomo kwa sababu anapenda sana shule. Nilimuahidi kuwa nitamsomesha mtoto huyo,” amesema Mavunde.

Baada ya kutembelea makazi ya familia hiyo na kujionea hali halisi ya maisha yao, Waziri Mavunde ameahidi kumjengea Scholastica nyumba ya matofali na kuiwekea umeme, hatua inayolenga kuwaondolea adha wanazokumbana nazo hususan kipindi cha mvua ambapo maji huingia ndani ya nyumba yao ya sasa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Julias Mtatiro amesema ofisi yake itashirikiana na Jeshi la Magereza kuhakikisha ujenzi wa nyumba hiyo unakamilika kwa wakati.

Ameongeza kuwa watoto watatu wa familia hiyo watapelekwa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ili wapatiwe elimu ya ufundi itakayowawezesha kujitegemea katika maisha yao ya baadaye.

Mtatiro pia ameahidi kusimamia matibabu ya watoto wawili wa familia hiyo wanaokabiliwa na changamoto za kiafya, pamoja na kuipatia familia hiyo mahitaji ya sikukuu.

Aidha, amesema familia hiyo itapatiwa fedha za kununua mbuzi 15 kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ufugaji utakaowaongezea kipato.

Akizungumza kwa hisia, Scholastica amesema kabla ya kupata msaada huo, maisha yao yalikuwa magumu hali iliyosababisha baadhi ya watoto wake kuathirika kiafya kutokana na ukosefu wa chakula.

“Maisha yangu yalikuwa magumu sana. Niliwakuza wanangu kwa shida kubwa, tulikuwa na changamoto ya chakula hadi kufikia kukaa siku moja au mbili bila kula. Hali hiyo ilisababisha watoto wangu kuugua matatizo ya tumbo,” amesema Scholastica.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa Waziri Mavunde kuona matokeo ya msaada alioutoa, pamoja na kuhakikisha familia hiyo inapatiwa msaada endelevu utakaoboresha maisha yao kwa ujumla.