Moshi. Mbuzi hashikiki. Ndivyo wafanyabiashara wa nyama ya mbuzi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wanavyoelezea hali ya soko katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, baada ya bei ya mnyama huyo kupanda kwa kasi akiuzwa kati ya Sh400,000 hadi Sh500,000 kwa mmoja mwenye uzito wa kilo 25 hadi 30.
Kupanda kwa bei hiyo kumeibua hisia mseto miongoni mwa wafanyabiashara na wananchi, huku mahitaji ya nyama ya mbuzi yakiongezeka lakini upatikanaji wake sokoni na kwenye minada ni mdogo.
Kwa sasa, mbuzi mmoja anauzwa kati ya Sh400,000 hadi Sh500,000, tofauti na miaka ya nyuma, alikuwa akiuzwa kati ya Sh200,000 hadi Sh300,000.
Hali hiyo imefanya bei kutoeleweka kwa wanunuzi wengi, hasa ikilinganishwa na misimu ya sikukuu iliyopita.
Mfanyabiashara wa nyama wilayani Moshi kwa muda mrefu, Peter Mselle akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Desemba 24, 2025, amesema mbuzi wa bei nafuu kwa sasa wanapatikana kwa shida na huuzwa kati ya Sh300,000 hadi Sh350,000 wakiwa na kilo chini ya 15.
“Kwa sasa mbuzi hawashikiki, wamepanda bei sana na hawapatikani kwa wingi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kwa mfano sasa hivi wanauzwa kati ya Sh450,000 hadi Sh500,000 na uzito wake ni kati kilo 25 hadi 30,” amesema Mselle.
Amesema ongezeko hilo la bei linatokana na uhaba wa mbuzi sokoni na katika minada mbalimbali.
“Hapo awali tulikuwa tunapata mbuzi wengi kutoka majumbani na minadani, lakini sasa wanapatikana kwa shida. Hata kwenye minada ya Kikatiti, Weruweru na Mgagao ambako tumezoea kwenda kununua, mbuzi ni wachache na bei iko juu sana,” amesema.
Mselle amesema katika misimu ya sikukuu iliyopita, machinjioni walikuwa wakichinja mbuzi kati ya 20 hadi 40 kwa siku, huku bei ya kununua ikiwa kati ya Sh120,000 hadi Sh200,000.
“Kwa sasa ukipata mbuzi wa Sh350,000 una bahati sana. Hali hii ikiendelea, kilo ya nyama ya mbuzi inaweza kufikia Sh14,000,” ameongeza.
Mkazi mwingine wa Kibosho, Wilaya ya Moshi, Deogratius Mushi amesema bei ya mbuzi imepanda kutoka Sh200,000 kwa mbuzi wa kawaida hadi kufikia Sh300,000, huku mbuzi mkubwa akiuzwa Sh400,000 hadi 500,000.
Amesema licha ya bei kupanda, pia wameadimika. “Leo nimeulizia mbuzi kwenye mnada wa Weruweru nimeambiwa mbuzi wa kawaida tuliyekuwa tunamnunua kwa Sh200,000 sasa anauzwa Sh300,000 na mbuzi mkubwa nimeambiwa anauzwa kati ya Sh400,000 hadi 500,000, bei ni kubwa sana,” amesema Mushi.
Kwa upande wa wafanyabiashara wa bidhaa nyingine, wamesema hali ya biashara imekuwa tofauti kulingana na aina ya bidhaa.
Dawsen Baraka, mfanyabiashara wa nafaka na viungo katika soko la Manyema, amesema mwaka huu wageni waliokuja kusherehekea sikukuu mkoani Kilimanjaro ni wengi, jambo lililoongeza idadi ya wanunuzi.
“Tunapata nafuu kwa sababu wageni ni wengi. Bidhaa zinazouzwa zaidi ni nafaka na viungo,” amesema Baraka.
Naye Aisha Matei, mfanyabiashara wa mazao ya chakula, amesema licha ya kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali, wanunuzi ni wengi.
“Mwaka jana kipindi kama hiki gunia la viazi lilikuwa linauzwa Sh110,000, lakini mwaka huu ni Sh140,000. Gunia la vitunguu lilikuwa linauzwa Sh90,000 hadi Sh100,000, sasa ni hadi Sh230,000 kwa gunia,” amesema.
Hata hivyo, si wafanyabiashara wote wanaotabasamu. Joyce Silas anayefanya biashara ya kuku si nzuri kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Kawaida kipindi kama hiki mauzo yanakuwa juu sana, lakini mwaka huu hali ni tofauti. Mauzo ni ya kawaida na nadhani hii inatokana na ugumu wa maisha unaolalamikiwa na wananchi wengi,” amesema.
Kwa upande wake, Japhet Masumbuko, mfanyabiashara wa samaki amesema biashara inafanyika kwa wastani.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Martin Tarimo, mfanyabiashara wa samaki soko la Manyema, ambaye amesema licha ya wingi wa watu sokoni, biashara ya mwaka huu haijafikia viwango vya miaka iliyopita.