Mahakama yafuta sharti Waislamu wote kutambulishwa na Bakwata

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imefuta sharti la Waislamu wote kutakiwa kuwa na barua ya Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) inayowatambulisha wanapohitaji kupata huduma mbalimbali hususan kusajili taasisi za kidini.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano, Desemba 24, 2025 na jopo la majaji watatu, Elizabeth Mkwizu (kiongozi wa jopo) Awamu Mbagwa na Hamidu Mwanga, kufuatia kesi ya kikatiba iliyofunguliwa mahakamani hapo na kikundi cha masheikh na walimu wa Dini ya Uislamu nchini.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 27603/2024 ilifunguliwa na Sheikh Ayoub Muinge, Sheikh Profesa Hamza Njozi, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzao wengine tisa wakiwemo waalimu (maustaadhi) wa dini hiyo, akiwemo mwanamke  Riziki Ngwali.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Msajili wa Jumuiya za Kijamii, Kabidhi Wasihi Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wadhamini waliosajiliwa wa Bakwata na Wadhamini wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.

Bakwata na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ziliunganishwa katika kesi hiyo kama ili kuwapa tu nafasi ya kujieleza kwa kuwa nazo ni taasisi zinazowahusu Waislamu.

Katika hati ya madai, wadai walikuwa  wanapinga kitendo cha Msajili wa Jumuiya na Kabidhi Wasihi Mkuu kuwalazimisha kuwa na barua inayowatambulisha kutoka Bakwata katika kusajili taasisi yoyote.

Hivyo pamoja na mambo mengine waliiomba mahakama hiyo itoe amri na tamko kuwa mwenendo na masharti yaliyowekwa na mdaiwa wa kwanza (Msajili wa Jumuiya) na wa pili (Kabidhi Wasihi Mkuu) katika usajili wa Jumuiya na taasisi ni ukiukwaji wa Katiba.

Walibainisha kuwa masharti hayo yanakiuka ibara za 13 (1), (2) na (3); 19(1) na (2); 20(1); 29(2) za Katiba ya Nchi.

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja pande zote katika hukumu yake leo imekubaliana na wadai kuwa Bakwata si chombo cha kuwawakilisha Waislamu wote isipokuwa wale tu wanaotajwa ndani ya Katiba ya Bakwata.

Imesema kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba ya Bakwata, dhehebu linalotajwa ni Shafii na Sunni Wal-Jamaa.

Hivyo mahakama hiyo imezitaka mamlaka hizo za Serikali kutokuchukulia sharti hilo la barua ya Bakwata kama takwa la kisheria  imezielekeza  kurekebisha utaratibu huo.

Akizungumzia hukumu hiyo, mmoja wa wadai katika kesi hiyo, Sheikh Ponda amesema shauri hilo lilikuwa ni la kudai uhuru wa Waislamu katika kujiamulia mambo yao wenyewe katika dini, kama vile uongozi, uanzishaji wa taasisi mbalimbali na hata umiliki wa mali.

Sheikh Ponda amesema kuwa hilo limekuwa ni tatizo kubwa ambalo Waislamu wamekuwa wakilipata nchini kwa kwa miaka mingi na kwamba wamekuwa wakilazimishwa wanapotaka uhuru katika masuala hayo kwamba hawawezi kuyafanya isipokuwa kwa kupata kibali cha Serikali kupitia Bakwata.

“Kwa maana hiyo hukumu hii ni taarifa rasmi kwa mamlaka zote za Serikali kwamba pale Waislamu wanapotaka kuomba huduma yoyote wasilazimishwe kwamba lazima walete barua kutoka Bakwata ndio wapewe hiyo huduma,” amesema Sheikh Ponda na kusisitiza;

“Kwa hiyo mamlaka zote za Waislamu na  Muislamu mmoja moja wamekuwa huru katika uanzishaji, umiliki au pale wanapotaka jambo lao lolote.”

Amesema hiyo ni hukumu ya kwanza kubwa kutolewa na kwamba wataandaa kongamano kubwa ambapo wanasheria watatoa ufafanuzi wataeleza umuhimu  wa hukumu hiyo na namna ambavyo Waislamu watanufaika nayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Sheria  Bakwata, Makao Makuu, Hassan Athuman amesema kuwa kimsingi wanakubali kuwa  Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini na Sheria ya Vyama vya Kijamii hazijasema kuwa kila bodi ya wadhamini au taasisi za Kiislamu zinaposajiliwa lazima zipate barua kutoka Bakwata.

“Na sisi tunajua hilo. Pengine ilikuwa ni sifa nzuri tu ya taasisi yetu ya Bakwata kuziagiza taasisi zinazotaka kusajiliwa, unajua hiyo introduction letter (barua ya utambulisho) inatakiwa itolewe na mtu anayekujua, maana Bakwata ni taasisi kongwe tangu mwaka 1968,” amesema Athuman na kufafanua zaidi:

“Kwa hiyo ilikuwa ni kama mazoea tu yaliyokuwa yakifanywa ma mujibu maombi wa kwanza (Msajili Vyama vya Kijamii) na wa pili (Kabidhi Wasihi Mkuu), kwamba kalete barua kutoka Bakwata, Lakini si takwa la sheria kama ambavyo mahakama imeliona.”

Kwa mukibu wa wakili wa wadai,  Juma Nassoro, sharti hilo lilikuwa linawalazimisha wateja wake kuwa chini ya Bakwata wakati hakuna sheria inayowalazimisha Waislamu wote kuwa chini ya Bakwata, ambayo yenyewe pia imesajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani na katika Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita).

Wakili Nassoro amesema kuwa kwa kuwa Bakwata na yenyewe imesajiliwa kama taasisi nyingine zilizosajiliwa, haina usajili wa kuwa taasisi  ya kuwawakilisha Waislamu wote nchini na kwamba hata Katiba yake (Bakwata) hakuna kipengele kinachobainisha ni nani mwanachama wa Bakwata.

“Kwa hiyo kuwalazimisha Waislamu wote kuwa chini ya Bakwata ni kinyume na Katiba (ya Nchi). Waislamu waachwe wenyewe waamue kuwa wanataka kuwa chini ya taasisi gani, na wanapotaka kusajili taasisi yoyote ya kidini wasilazimishwe kwamba watambuliwe na Bakwata,” amesema Wakili Nassoro.

Amesema kuwa wanapaswa waulizwe wao wenyewe na kwamba kama ni lazima walete barua ya taasisi iliyosajiliwa ya Kiislamu inayowatambua, waulizwe wao wenyewe wanaotaka kusajili taasisi yao kuwa wanataka taasisi gani iwatambue.

“Lakini siyo kuwalazimisha kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa mtu yeyote kujiunga na jumuiya yoyote anayoitaka. Sasa huwezi kuwalazimisha wote wawe chini ya Bakwata, hiyo ni kuvunja Katiba:, amesema wakili Nassoro na kusisitiza:

“Kwa hiyo walikuwa  wanavunja Katiba, lakini pili hakuna sheria yoyote inayowataka Rita au Msajili wa Vyama vya Kijamii kuwaelekeza Waislamu waende Bakwata wakalete barua.”