Bao la Dube AFCON laibua makocha

MSHAMBULIAJI Prince Dube amefunga bao flani la kihistoria wakati timu ya taifa ya Zimba-bwe ikilala kwa mabao 2-1 mbele ya Misri katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea huko Morocco na kuwaibua makocha wawili waliotoa ushauri kwa klabu ya Yanga.

Dube mwenye mabao mawili Ligi Kuu Bara kwa msimu huu, alifunga bao hilo la utangulizi na lililokuwa la kufutia machozi kwa Zimbabwe katika Kundi A na la kwanza kwake katika michuano hiyo ya 35 inayohusisha nchi 24 ikiwamo Tanzania inayoshiriki kwa mara ya nne tangu 1980.

Katika mechi hiyo iliyopigwa majuzi, Dube alifunga baada ya kupokea krosi ya upande wa kulia kutoka kwa beki Emmanuel Jalai kisha akiwa amezungukwa na mabeki wa Misri akitu-mia mguu wa kulia kisha akageuka kiufundi na kufunga kwa mguu wa kushoto dakika ya 20.

Bao hilo limewashangaza baadhi ya wadau waliozungumza na Mwanaspoti kwa namna Dube alivyolifunga kisasa, akiwamo kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Rob-ertinho’ pamoja na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi Yanga ambao kila mmoja alitoa maoni tofauti.

Robertinho alisema mshambuliaji huyo licha ya kukutana na ukame wa mabao, anatakiwa kujengwa kisaikolojia atakaporudi klabuni ili aweze kuendeleza makali aliyonayo akisema Dube ni mshambuliaji mwenye ujuzi wa kufunga.

“Dube alifunga bao zuri, niliangalia ile mechi, namna alivyopokea mpira na kugeuka na aka-funga sio rahisi kwa beki kuelewa akili yake, alifanya mambo kwa haraka sana,” alisema Dube na kuongeza;

“Ni kweli naona kuna wakati anakuwa hafungi klabuni kwake Yanga, lakini nadhani ni pre-sha tu, anaichezea timu yenye presha kubwa, makocha wake na hata viongozi wanaweza kumsaidia kwa kumlinda anapokutana na presha ya namna hiyo kutoka nje ya uwanja.”

Kocha Nabi kwa upande wake alisema anajua Dube alitoka timu isiyo na presha kubwa (Azam FC) na kwenda Yanga ambayo wakati wote presha ya matokeo ni kubwa, lakini bao alilofunga linathibitisha kwamba jamaa ni mshambuliaji mwenye akili.

Nabi ambaye wakati anatua Yanga katika mechi ya kwanza ya kukaribishwa katika Ligi Kuu alivaana na Azam na Dube ndiye aliyemfunga kwa shuti la mbali lililomshinda nguvu kipa Farouk Shikhalo na kumtibulia kocha huyo, alisema anaamini Mzimbabwe huyo kama ataondoa hofu anapokuwa na klabu yake anaweza kufunga zaidi.

“Wakati Yanga inacheza na FAR Rabat, nilizungumza na kiongozi mmoja wa Yanga, akaniambia wasiwasi wao ulikuwa kule mbele na hakuwa na imani na Dube, lakini ni yeye ndiye  alifunga bao la ushindi kwenye Uwanja wa New Amaan katika mechi hiyo ngumu na muhimu,” alisema Nabi na kuongeza;

“Angalia tena katika mechi ngumu kama ya Misri anafunga bao lingine bora akiwasumbua mabeki kwa akili kubwa, ni muendelezo mzuri, kitu cha kwanza ambacho Dube anatakiwa kufanya ni kuhakikisha anaiondoa presha kwenye akili yake anapokuwa Yanga.”

Nabi aliongeza kwa kusema; “Mimi nimefanya kazi Yanga ninaelewa joto analokutana nalo kama anaweza kucheza mechi mpaka tatu au zaidi bila kufunga, lakini anaweza kusaidiwa na mashabiki na hata  uongozi wake wajue kwamba wana mshambuliaji mzuri wasimsham-bulie sana anapokuwa hafungi.”

“Najua makocha wanamsaidia sana kisaikolojia, wanatakiwa kuendelea kumjenga zaidi kwa kuwa wameshaona akiwa hana presha anakuwa bora kwa kiwango kikubwa kama hivi sasa. Kwa namna alivyofunga kwenye hizi mechi kubwa, akiendelea kuimarika zaidi anaweza kufunga mabao zaidi.”

Huu ni msimu wa pili kwa Dube akiwa na kikosi cha Yanga kwani mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, ambapo kwa msimu uliopita alimaliza na mabao 13 katika Ligi Kuu na kwa mwaka huu unaomalizika ameifungia timu ya taifa ya Zimbabwe mabao mawili katika mechi tofauti likiwamo moja la Afcon 2025.