Morogoro. Jamii imetakiwa kuongeza uelewa na kuchukua hatua za makusudi katika kukata bima za vyombo vya moto kama njia ya kujilinda dhidi ya majanga yanayotokana na ajali za barabarani ambazo hurudisha nyuma maisha ya watu kiuchumi na kijamii.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa kampuni ya bima ya Bumaco Insurance Ltd tawi la Morogoro, Faith Boma alisema bado jamii ina uelewa mdogo kuhusu sera na sheria za bima ya vyombo vya moto hali inayosababisha wengi kushindwa kudai haki zao pindi ajali zinapotokea.
Alisema bima ya vyombo vya moto imegawanyika katika matumizi binafsi na ya kibiashara huku upande wa biashara ukihusisha magari ya kubeba abiria na mizigo ambayo kila moja ina masharti yake kulingana na matumizi.
Kwa mujibu wa Faith, bima ndogo (Third Party Insurance) ni ya lazima kisheria kwa kila chombo cha moto, huku bima kubwa ikibaki kuwa hiari lakini yenye faida kubwa kwa mmiliki wa gari.
Akitolea mfano, alisema kwa basi la ndani ya mkoa lenye siti 65, bima ndogo hukatwa kwa wastani wa Sh15,000 kwa kila siti, sawa na Sh975,000 kwa mwaka ambapo ikiongezwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya asilimia 18 ya Sh175,500 basi mmiliki hulipa jumla ya Sh1,150,500 kwa mwaka.
Kwa basi ndogo aina ya coaster, Tata lenye siti 18 linalofanya safari za kibiashara, bima ndogo hukatwa kwa wastani wa Sh30,000 kwa kila siti sawa na Sh540,000 kwa mwaka na inapoongezzwa (VAT) ya 18 ambayo ni Sh97,200, jumla ya malipo hufikia Sh637,200 kwa mwaka.
“Bima kubwa huhesabiwa kwa kuzingatia thamani ya gari, idadi ya siti na kodi ya asilimia 18, hii humlinda mmiliki dhidi ya hasara kubwa endapo gari litapata ajali, kuungua au kuharibika kabisa,” alisema.
Kwa upande wake, mdau wa usafiri Frank Kasele alisema baadhi ya abiria hukosa fidia kwa kukosa tiketi au risiti kutokana na ulipaji wa nauli pungufu, jambo linalowafanya wasitambulike kisheria kuwa walikuwa kwenye basi husika.
Aliitaka Latra na wamiliki wa mabasi kuboresha mifumo ya tiketi ili kumlinda abiria na kumpa nguvu ya kudai haki zake.
Meneja wa Latra Mkoa wa Morogoro, Andrew Mlacha alisema mamlaka hiyo imeanzisha mifumo ya kielektroniki ikiwamo Safari Tiketi App na City S App inayohifadhi kumbukumbu za abiria na mizigo hivyo kurahisisha ulipaji wa fidia pindi ajali zinapotokea.