TMDA yaimarisha ulinzi dawa zenye asili ya kulevya

-Waganga wafawidhi, wafamasia wapigwa msasa kuzuia uchepushaji

Na MASHAKA MHANDO, Tanga

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imetoa mafunzo maalum kwa Waganga Wafawidhi, Wafamasia na Wakaguzi wa dawa kutoka wilaya nne za Mkoa wa Tanga, lengo likiwa ni kudhibiti matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya (Narcotics & Psychotropics) ili kuzuia uraibu miongoni mwa vijana.

Mafunzo hayo yaliyolenga wilaya za Tanga Jiji, Muheza, Pangani na Mkinga, yanakuja kama mkakati wa Serikali kuhakikisha dawa hizo kali ambazo ni muhimu kwa wagonjwa wa upasuaji na saratani, haziingii mitaani kinyume cha sheria.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa TMDA Kanda ya Mashariki, Keddy Manga, alisema kuwa jukumu la msingi la mamlaka hiyo ni kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni bora, salama na vina ufanisi, lakini tahadhari kubwa inahitajika kwenye dawa za maumivu makali.

“Kuna dawa zinatumika kwa wagonjwa wenye maumivu makali kama wa saratani au wanaofanyiwa upasuaji. Hata hivyo, dawa hizi zisipotumika kwa usahihi na kwa kufuata miongozo, zinaweza kusababisha uraibu na kugeuka kuwa dawa za kulevya mitaani,” alisema Manga.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Japhet Simeo, alifichua kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bombo kwa sasa inahudumia zaidi ya wagonjwa 700 walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya.

Dkt. Simeo alionya kuwa baadhi ya wataalamu wasio waaminifu wamekuwa wakichepusha dawa hizo na kuzipeleka mitaani, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa Taifa na nguvu kazi ya vijana.

“Serikali imeweka utaratibu maalum wa matumizi ya dawa hizi. Wataalamu wetu hawana budi kufuata mwongozo wa udhibiti ili dawa za upasuaji na zile za afya ya akili zisichepushwe. Matumizi bila maelekezo ya daktari ni sumu inayozalisha waraibu mitaani,” alisisitiza Mganga Mkuu huyo.

Naye Mfamasia wa Mkoa wa Tanga, Beatha Kimaro, alibainisha kuwa mkoa umeanza kuweka mifumo thabiti ya utunzaji wa dawa hizo chini ya watu maalum (Double-lock system) ili kuzuia mianya ya uchepushaji.

Alizitaja baadhi ya dawa zinazofuatiliwa kwa ukaribu kuwa ni pamoja na zile za jamii ya *Psychotropic*, *Narcotics* kama vile Pethidine na Morphine, pamoja na Diazepam (Valium), ambazo zote zina uwezo mkubwa wa kuleta uraibu kama zitatumika vibaya.

Mafunzo hayo yamepokelewa kama mkombozi katika usimamizi wa dawa mkoani Tanga, huku TMDA ikisisitiza kuwa itaendelea na ukaguzi wa kushtukiza katika vituo vyote vya afya na maduka ya dawa ili kuhakikisha sheria inafuatwa bila upendeleo.