Arusha. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel amewataka wazai na walezi kutumia sikukuu za mwisho wa mwaka vizuri huku wakitambua Januari wana wajibu wa kupeleka watoto shule.
Aidha amewatoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) maarufu kama Selian inayomilikiwa na kanisa hilo, ambapo kuanzia Desemba 29, 2025 hadi Januari 2026 kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) watatoa huduma za kupima moyo bure.
Dk Mollel ameyasema hayo leo Alhamisi Desemba 25, 2025 na Askofu huyo, wakati akitoa salamu za Sikukuu ya Krismasi katika Usharika wa Arusha Mjini, Kanisa Kuu (Cathedral).
Amesema leo ni sikukuu ya kufurahia na familia pamoja na kuwakumbuka watu wenye mahitaji mbalimbali na kuwataka wazazi na walezi kula, huku wakitambua Januari watoto wanapata mahitaji muhimu ya shule.
“Tunaomba Mungu leo iwe siku ya amani katika familia, kweli ikawe amani, leo ni siku hata ya kubadilisha mlo jamani tukale kwa furaha, leo siyo siku ya ujinga ni siku ya kufurahi na familia. Tunapokula tukumbuke Januari shule, tule kwa akili tuwapeleke watoto shule,” amesema Dk Mollel.
“Leo natoa tangazo la kuwahimiza watu kuanzia Desemba 29 mfike pale hospitali ya Kanisa ya Selian,mfike kwa wingi uwe na kadi ya bima usiwe nayo,ili mradi wewe ni mwanadamu ufike ukapimwe moyo,” amesema.
Kuhusu vipimo hivyo Askofu huyo aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupima afya zao.
“Kwa hiyo kutakuwa na vipimo vya moyo na wataalam wetu wa JKCI na ALMC, watafanya kazi hiyo hadi Januari 5,2026 na ukikutwa na shida inayohitaji dawa utapewa, tuachane na ile dhana kwamba hospitali haina dawa,”
Awali, akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Desemba 16, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema taasisi hiyo imeingia makubaliano ya uendeshaji wa hospitali hiyo kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.
Amesema hatua hiyo imelenga kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambapo makubaliano ya ubia huo yanaifanya ALMC kuwa tawi la tano linaloendeshwa na taasisi hiyo.
Alieleza utekelezaji rasmi wa makubaliano hayo utaanza kwa kambi kubwa ya kuwapima wananchi magonjwa ya moyo lengo likiwa kuwafikishia wananchi huduma za kibingwa karibu badala ya kutumia gharama kubwa kuzifuata Dar es Salaam.
