Askofu Chakupewa: Siasa za udini zinachochea migogoro, hazifai

Tabora. Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Tabora, Elias Chakupewa amesisitiza kutofanya siasa za udini kwani zinachochea migogoro miongoni mwa madhehebu ya dini na jamii kwa ujumla.

Amesema hayo leo Alhamisi Desemba 25,2025 wakati akizungumza na waumini wa kanisa hilo katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi, huku akisisitiza kusherehekewa sikukuu hiyo kwa amani na utulivu.

“Acheni kabisa mambo ya kuingiza udini kwenye siasa kwani inachochea migogoro miongoni mwetu, hii sio asili ya Tanzania kuwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kwani tumezoea amani, upendo na mshikamano”amesema Askofu Chakupewa.

Amesema sikukuu hiyo ikawe ni sababu ya kudumisha heshima ya madhehebu ya dini na kuacha kugeuza majukwaa ya dini kurushiana maneno yanayoshusha heshima ya dini nyingine au utu wa mtu kwani sio desturi na mila za Watanzania.

Ameongeza kuwa   Tanzania ni mfano wa kuigwa  kwa namna lilivyoweza kuidumisha amani yake na kuwa kimbilio la baadhi ya mataifa ambayo yamekua na migogoro ya muda mrefu, hivyo isiwe rahisi kuichezea amani iliyopo.

“Sisi tuliobahatika kutembea kwenye nchi mbalimbali tunaweza kusimulia vizuri madhara ya machafuko kwani hakuna kinachoweza kufanyika kwa ajili ya maendeleo ya Taifa au kukaa kwa kutulia na kupanga mipango kwa ajili ya maendeleo, hivyo tusirahisishe tu suala la kuharibu amani ya nchi.”

Aidha Joel Minigwe mkazi wa Tabora amesema jambo kubwa ili kufanikiwa kuendelea kuimarisha amani nchini ni muhimu kuwa na matumizi bora ya mitandao ya kijamii, kuacha kutuma maudhui yasiyofaa yanayomchafua  watu au madhehebu yao ya dini.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,  Richard Abwao amewahakikishia ulinzi na usalama wananchi mkoani humo katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.