Lybia. Ajali ya ndege iliyotokea katika ardhi ya Uturuki imesababisha kifo cha Mkuu wa Jeshi la Libya, Jenerali Muhammad al-Haddad, maofisa wengine wanne pamoja na wahudumu wa ndege watatu.
Muda mfupi baada ya kutokea ajali hiyo na kuwatambua waliokuwemo, Jana Jumatano Desemba 24, 2025, Rais wa Uturuki, Recep Erdogan ametuma salamu za rambirambi kwa kiongozi wa Lybia akiwatakia pole kwa msiba huo uliowakuta.
“Tayari uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hili la kusikitisha sana ambalo limetuhuzunisha kwa kiasi kikubwa, na wizara zetu zitatoa taarifa kuhusu maendeleo ya uchunguzi huo,” amesema Rais Erdogan.
Timu za utafutaji siku ya Jumatano zilifanikiwa kurejesha kinasa sauti cha chumba cha rubani na kifaa cha kurekodi taarifa za safari ya ndege huku juhudi za kurejesha miili ya waathiriwa zikiendelea, amesema Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki.
Ndege binafsi iliyombeba Jenerali Muhammad Ali Ahmad al-Haddad, maofisa wengine wanne wa kijeshi na wahudumu watatu wa ndege ilianguka nchini Uturuki siku ya Jumanne baada ya kuondoka katika mji mkuu, Ankara, na kuua watu wote waliokuwemo ndani.
Mabaki ya ndege yalipatikana karibu na kijiji cha Kesikkavak, eneo la Haymana, wilaya iliyo takriban kilomita 70 (maili 45) kusini mwa Ankara.
Maofisa wa Libya walisema chanzo cha ajali hiyo kilikuwa hitilafu ya kiufundi katika ndege.
Ujumbe huo wa ngazi ya juu kutoka Libya ulikuwa ukirejea Tripoli baada ya kufanya mazungumzo ya ulinzi mjini Ankara, yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili.
Ujumbe wa watu 22 wakiwemo wanafamilia watano uliwasili kutoka Libya mapema Jumatano kusaidia katika uchunguzi.
Al-Haddad alikuwa kamanda mkuu wa jeshi katika magharibi mwa Libya na alichukua jukumu muhimu katika juhudi zinazoendelea, zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa, za kuunganisha jeshi la Libya, ambalo limegawanyika kama taasisi nyingine za nchi hiyo.
