Zanzibar yajivunia uwenyeji mashindano ya Africa Sports Federation

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema inajivunia kuwa mwenyeji wa mashindano ya Africa Sports Federation ambayo yanafanyika visiwani hapa kwa mara ya kwanza.

Mashindano hayo ya 47, yanashirikisha wanamichezo 300 kutoka jumuiya za Khoja Shia Ithnashir duniani wakiwamo wanaume na wanawake yanayolenga kukuza michezo Zanzibar ambapo tamati ni Desemba 28, 2025.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, usiku wa kuamkia Desemba 25, 2025 wakati akifungua tamasha hilo, linalofanyika katika viwanja vya Maisara Sports Complex.

Rais Mwinyi, amesema michezo ni nyenzo muhimu na alama ya kuwaunganisha watu wa jamii na mataifa mbalimbali katika kuimarisha ushirikiano, upendo na umoja. 

“Zanzibar inajivunia kuwa mwenyeji wa mashindano haya kwa mara ya kwanza yakishirikisha wanamichezo 300 kutoka jumuiya mbalimbali za Khoja Shia Ithnashir duniani, hili ni jukwaa muhimu la kuleta furaha, upendo, mshikamano na kukuza michezo,” amesema. 

Dk Mwinyi, ametoa wito kwa wanamichezo kushiriki mashindano hayo kwa kuonesha upendo na uhusiano mwema ili kuyafanya kuwa ya mafanikio, sambamba na kutumia fursa ya kutembelea vivutio vya utalii na maeneo ya kihistoria ya Zanzibar.

Aidha, ameipongeza Africa Sports Federation kuandaa semina ya wawekezaji itakayojadili fursa za kiuchumi na uwekezaji zilizopo Zanzibar kwa wageni wanaoshiriki mashindano hayo kutoka mataifa mbalimbali.

Awali, Katibu wa Jumuiya ya Islam Jammat ya Zanzibar, Hassan Mohamed Raza, amesema kufanyika kwa mashindano hayo Zanzibar kumechangiwa na uwepo wa miundombinu ya kisasa ya michezo, ikiwemo viwanja bora.