Afariki ajalini Tanga akielekea Moshi, wanne wajeruhiwa

Tanga. Safari ya kusherehekea sikukuu ya Krismasi mjini Moshi imegeuka majonzi baada ya dereva wa gari dogo, Justine Jacobo Njau (32), kufariki dunia papo hapo na wengine wanne wakijeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea alfajiri ya Desemba 25, 2025, mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, ajali hiyo ilitokea saa 10:30 alfajiri katika Kijiji cha Taula, Wilaya ya Handeni, kwenye barabara kuu ya Chalinze kuelekea Segera.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linafanya uchunguzi wa ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 25 Desemba 2025, saa 10:30 alfajiri, katika Kijiji cha Taula, Wilaya ya Handeni, kwenye barabara kuu ya Chalinze kuelekea Segera,” amesema Kamanda Mchunguzi.

Amesema ajali hiyo ilihusisha gari dogo aina ya Toyota Runx lenye namba za usajili T 350 DZA lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Moshi na gari la mizigo aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 857 DZK lililokuwa likitokea Segera kuelekea Chalinze.

“Katika tukio hilo, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Justine Jacobo (32), aliyekuwa dereva wa Toyota Runx, amepoteza maisha papo hapo. Aidha, watu wengine wanne wanaume wawili na wanawake wawili, akiwemo mtoto mmoja wamejeruhiwa na wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini,” amesema.

Kwa mujibu wa polisi, uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha ajali kuwa ni uzembe wa dereva wa Toyota Runx aliyefanya jaribio la kuyapita magari mengine (overtaking) katika eneo lisiloruhusiwa bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na gari la mizigo.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ha simu,baba mdogo wa marehemu, Adam Njau, amesema familia imepokea kwa majonzi taarifa za kifo cha Justine, aliyekuwa anakwenda Moshi kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Krismasi pamoja na marafiki zake wanne.

“Ni kweli tumempoteza Justine. Alikuwa anatokea Dar es Salaam akija Moshi kwa ajili ya sikukuu. Taarifa tumezipokea asubuhi na baadhi ya wanafamilia wameanza taratibu za kufuatilia hatua zinazofuata,” ameema Adam Njau.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limewataka madereva kuacha kuendesha kwa kasi na kufanya maamuzi hatarishi barabarani, hasa katika kipindi cha sikukuu. Polisi wamesisitiza kuzingatiwa kwa kauli mbiu ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani inayosema, “Endesha salama, familia inakusubiri.”