Dar/mikoani. Sikukuu ya Krismasi imetamatika, huku viongozi wa kiroho wakitaka itumike kuwa chachu ya kuzika tofauti na kujenga utayari wa kuanza upya, wakisisitiza kukomeshwa kwa ufisadi, ukatili, ulafi, ibada za uongo, hasira na fitina.
Katika baadhi ya madhabahu, sikukuu hiyo na ile ya Mwaka mpya, viongozi wa makanisa wametaka ziwe mwanzo wa jamii kuthamini uhai na yeyote asifikirie kuutoa wa mwingine, kwa kuwa kufanya hivyo ni kuingilia mamlaka ya Mungu.
Mahubiri ya viongozi hao wa dini katika sikukuu hiyo ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo yalihusisha onyo kwa waliopata nafasi za uongozi, kuhakikisha wanakuwa wanyenyekevu na wazitumie nafasi hizo kuwahudumia waliowawezesha kuzipata.
Hayo yameelezwa leo, Alhamisi, Desemba 25, 2025, na viongozi mbalimbali wa dini ya Kikristo kwa nyakati tofauti, katika mahubiri yao wakati wa ibada ya Sikukuu ya Krismasi.
Ibada ya kitaifa, unyenyekevu
Katika Ibada ya kitaifa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Bikira Maria Mshindani, Kigoma, Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Joseph Mlola, amesema Mungu aliichagua Krismasi kuwa siku ya unyenyekevu dhidi ya kiburi, upendo dhidi ya chuki na huduma dhidi ya utawala.
Kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika hali duni, amesema, kunawafundisha binadamu kwamba ukuu hupatikana katika unyenyekevu, huruma na kuwahudumia wengine.
“Tulipokee, tulielewe na tuliishi kwamba tunapotafuta nafasi mbalimbali kwenye jamii, tukumbuke huduma, Yesu amekuja kwetu kwa ajili ya kuhudumia na siyo kuhudumiwa,” amesema.
Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Joseph Mlola. Picha na Mtandao
Msisitizo wa Askofu Mlola ni kile alichoeleza kuwa ni muhimu kila mtu awe mnyenyekevu, awe na huruma na aweke kipaumbele kuwahudumia wale waliompa nafasi aliyonayo.
“Kazi ya mfalme ni kutawala na kuongoza. Kristo amekuja kutawala maisha yetu na kutuongoza kwa Mungu. Amekuja kuanzisha utawala wa Mungu duniani wa haki, amani, umoja na upendo,” amesema.
Ameeleza ni vigumu binadamu kuishi kumfikia Yesu, lakini angalau somo la unyenyekevu wake linawaalika watu kufanya jambo fulani.
“Mara ngapi tukiwa katika hali zetu za kawaida tunakimbizana na majukumu katika maeneo yetu, kwa nini tunapopata nafasi fulani tunaanza kupandisha mabega, tunaanza kuona hata tuliokuwa nao pamoja kwamba hatuwafahamu tena?” amesema.
Ameeleza ni muhimu kujifunza unyenyekevu, vyeo na nafasi zisiwe sababu za kung’ang’ania kwa nguvu, bali kujishusha ili kuwafikia wale wanaopaswa kuhudumiwa.
“Si kuanza kudharau, kuona kwamba wale ni duni na wewe ulikuwa humo. Waswahili wanasema, mpanda ngazi hushuka,” amesema Askofu Mlola.
Askofu huyo amesema Yesu huonekana kwa maskini wanaohitaji msaada, wagonjwa wanaohitaji huduma, vijana wanaohitaji kusikilizwa katika hofu na mihangaiko yao ya maisha, wazee wanaohitaji heshima na matunzo, familia zinazopitia changamoto na magumu ya kiuchumi na maisha kwa ujumla.
“Hawa wote wanahitaji matumaini mapya ya mtoto aliyezaliwa, tumuenzi Masihi aliyezaliwa kati yetu kwa kutenda mema na kukwepa dhambi, na Mungu atatujaza baraka na neema zake,” amesema.
Ametumia madhabahu hiyo pia kueleza ujumbe wa amani unaoihusu dunia nzima na kwamba inampasa binadamu kueneza amani kuanzia katika nafsi yake, familia, Taifa na ulimwengu kwa ujumla.
“Lakini daima ianzie kwetu, mtu mmoja mmoja, na kila mmoja ajitahidi kuwa chombo cha amani ya Mungu. Yesu ni Mfalme wa amani, alikuja kuleta amani na haki pale ambapo haikuwepo, ni sisi tunapaswa kujitahidi iwepo,” amesema.
Askofu Mlola amesema Mungu anafundisha kutambua thamani ya uhai, hivyo yeyote asifikirie kuutoa uhai wa mwingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kuingilia mamlaka yasiyo yake.
“Mtu yeyote asiote ndoto, iwe ya mchana au usiku, katika maisha yake au kufikiria tu kuutoa uhai wa mwenzake au hata uhai wake mwenyewe, ambao kimsingi si wake bali ni mali ya Mungu.
“Mwenye mamlaka ya uhai huo yupo, tusijitwalie jukumu lisilotuhusu, tuwe na hofu ya Mungu maishani mwetu. Uhai wa mtu unaanza tangu pale kutungwa mimba mpaka pale Mungu atakapoamua kuutoa.”
Amesema kufikiri na kutenda kinyume na ukweli huo ni kukosa hekima inayotaka kuchagua yaliyo mema na kuacha mabaya ya uovu.
Kuzaliwa kwa Yesu, amesema, kutukumbushe wajibu wa kila mmoja kulinda uhai na haki ya kila mmoja kuishi.
Kuzika tofauti, kuanza upya
Katika mahubiri yake hayo, Askofu Mlola amesema ni muhimu kuwa tayari kuanza upya katika maisha na daima tusikubali kubaki sehemu moja, kwani binadamu anapaswa kubadilika.
“Kama tulikuwa na mahusiano mabaya, hatuelewani, tuanze maisha mapya, kama tulikuwa na tabia mbaya, tuanze upya. Krismasi ni mwanzo mpya. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo ni mwanzo mpya wa maisha,” amesema.
Ametaka watu kuwa tayari kuzika tofauti kwa kuhakikisha visababishi vya kutofanana na Mungu vinang’olewa, ikiwemo ukatili, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada za uongo, uchawi, hasira, fitina, uzushi, husuda, ulevi na ulafi.
Ameitaka jamii kushikamana na masuala ya kiroho yatakayoipeleka katika uzima, upendo, haki, amani, uvumilivu, furaha, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi.
“Njia rahisi ya kuishi hayo na kuishi vizuri na Mungu na jirani, usimtendee mwenzako kile ambacho hupendi wewe mwenyewe utendewe. Kama unaona maisha yako ya thamani na unayapenda, basi usifikirie kudhuru maisha ya mwenzako,” amesema.
“Kama unapenda nyumba yako ibaki salama, usijiingize kwenye mambo ya kuharibu nyumba za wengine, kama unapenda upendwe, upende pia wengine, kama unapenda utendewe haki, utende haki kwa wengine na utambue pale inapoishia haki yako inaanza haki ya mwenzako hakuna sababu ya kukanyaga haki ya wengine,” amesema.
Pia, amesema Yesu ameomba afanywe kuwa chombo cha amani na kueneza mapendo wanapochukiana, msamaha wanapokosana, apatanishe wanapogombana, atumainishe wanapokata tamaa, awashe taa penye giza, alete furaha kwenye huzuni.
“Bahati mbaya, wakati mwingine tunashindwa kuyaona maneno haya ya busara, hekima maneno ya kutufanya tutembee pamoja, hasa pale ambapo tunatumia nafasi zetu vibaya badala ya kuleta mapatano tunaongeza petrol, badala ya kuleta furaha tunazidisha huzuni hiyo haituachi salama,” amesema.
Ametaka aombwe Mtakatifu Francisco ili awafanye watu kuwa vyombo vya amani, haki na kuwa sababu ya kuleta upendo, upatanisho na matumaini pale ambapo kuna hali ya kukata tamaa.
“Mungu tujaalie kufariji kuliko kufarijiwa, kufahamu kuliko kufahamika, kupenda kuliko kupendwa, anayetoa atapokea, anayesamehe atasamehewa, anayekufa kwa ajili ya Kristo atazaliwa kwenye uzima wa milele,” amesema.
Katika mahubiri yake wakati wa mkesha huo katika Kanisa Kuu la Azania Front, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa, amesema Kristo amewataka waumini waishi kwa kudumisha amani hata kama watu watabeza hilo, ndiyo hitaji na dai lake.
Amesema hata malaika na jeshi la mbinguni walitangaza kwa kupaza sauti: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni na amani duniani kwa watu wote.”
“Najua kama Taifa tumepitia katika kipindi kigumu, ambacho sina hakika kwa wale wanaonizidi umri kama wamewahi kupita kipindi kigumu kama hiki, hakuna hatujui kwa nini,” amesema Askofu Malasusa.
Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa baada ya kumalizika ibada ya Krismasi iliyifanyika Kanisa la Azania Front leo Alhamisi Desemba 25, 2025
Amesema watu wa kiroho wamekuwa wakijiuliza kwa nini Mungu ameruhusu mambo hayo kutokee, akisema tafsiri ni nyingi, lakini mojawapo ni Mungu kutaka kuonesha umuhimu na thamani ya amani. Watu wanaposikia amani, watambue maana yake.
Amesema anajua wapo wengi walihuzunishwa na vifo vingi na wengine wamehuzunishwa kuharibika kwa mali, na wao, kupitia Krismasi, waseme “Atukuzwe Mungu juu mbinguni na amani hapa duniani na Tanzania ikatawale.”
“Ndugu zangu, ni vigumu sana kupata maneno yanayoweza kuelezea umuhimu wa amani, ni vigumu sana, lakini itoshe tu kuwa Mungu wa Krismasi na huyu Yesu anayezaliwa, yeye ambaye ni Mfalme wa amani, atawale kwanza katika mioyo yetu,” amesema Askofu Malasusa.
Askofu huyo amesema amani nyingine zinazotokana na bunduki na risasi ziendelee, lakini kubwa ni amani moyoni. Kukiwa na amani hiyo kutakuwa na baraka hata ndani ya familia.
Katibu wa Askofu wa Kanisa la Mtakatifu Yosefu, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Vicent Mpwaji, amesema laiti binadamu angetambua cheo au wadhifa aliopewa, basi dunia ingeishi katika amani na utulivu.
“Tunaposheherekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo, tunakumbushwa kuiishi hadhi kubwa na ya kipekee ambayo Mungu ametupatia pasipo mastahili yetu, kumkomboa mwanadamu ili tuweze kuishi maisha ya Kimungu,” amesema.
Amewahimiza kutumia nuru na neema ambayo Mungu amewapatia kuwa wasikivu, waelewa na watekelezaji wa maagizo ya Mungu.
“Hakika ni jambo la kushangaza kuona mtu yuko tayari kutembea gizani ilhali ameshika tochi mkononi, hilo hufanyika kutokana na ukaidi wa mioyo ya sisi wanadamu,” amesema Padri Mpwaji.
Katika mahubiri yake, Kasisi Kiongozi wa Kanisa Kuu la Anglikana Mtakatifu Albano, Dayosisi ya Dar es Salaam, Christian Nchimbi, amesema Krismasi ni kipindi muhimu cha kujitafakari na kuingia katika mapatano na upatanisho.
Amesema maisha ya Yesu Kristo yalijengwa juu ya msingi wa kuwapatanisha watu ili waishi kwa umoja na amani.
“Krismasi iwe mwanzo wa watu kupatana na kuachana na tofauti zao. Ni wakati wa kuangalia tulipokoseana, kupata nafasi ya kupatana na kuwa wapatanishi wa kweli katika maisha yetu na ya wengine,” amesema.
Amesema kuzingatia mapatano, upendo na amani ni tafsiri halisi ya kuupokea kusudio la Mungu, jambo litakalosaidia jamii kuishi kwa kujali na kuheshimiana nyakati zote.
Msing’ang’anie madaraka
Mchungaji wa Kanisa Anglikana Mtakatifu Marko Sofu, mkoani Pwani, Rogers Mshuza, amewaonya viongozi wanaopenda kung’ang’ania madaraka kuacha tabia hiyo akisema inaleta chuki, migawanyiko na machafuko katika jamii na duniani kwa ujumla.
Amesema kila uongozi una ukomo wake na haupaswi kuchukuliwa kama wa milele, akiwataka kutambua madaraka ni dhamana ya muda iliyowekwa na Mungu, si mali binafsi ya mwanadamu.
Amesema historia ina mifano wazi inayoonesha madhara ya tamaa ya madaraka, akitolea mfano Mfalme Herode aliyekuwa mtawala wa Wayahudi, aliyefikia hatua ya kuamuru watoto wachanga wa kiume wachinjwe kwa hofu ya kupoteza cheo chake.
Ameeleza kuwa matukio hayo ni funzo kwa viongozi wa nyakati zote kuwa tamaa ya madaraka husababisha maamuzi yasiyo ya haki na kuvuruga amani ya jamii.
Tukumbuke wajibu wa Januari
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel, amewataka wazazi na walezi kutumia sikukuu za mwisho wa mwaka vizuri huku wakitambua kuwa Januari wana wajibu wa kupeleka watoto shule.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel. Picha na Mtandao
“Tunaomba Mungu leo iwe siku ya amani katika familia, kweli ikawe amani. Leo ni siku hata ya kubadilisha mlo, jamani tukale kwa furaha, leo siyo siku ya ujinga, ni siku ya kufurahi na familia. Na tunapokula, tukumbuke Januari shule, tule kwa akili tuwapeleke watoto shule.
“Leo natoa tangazo la kuwahimiza watu kuanzia Desemba 29, wafike kwa wingi pale hospitali ya Kanisa ya Selian, uwe na kadi ya bima au usiwe nayo, ili mradi wewe ni mwanadamu, ufike ukapimwe moyo,” amesema.
Askofu wa Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Tabora, Elias Chakupewa, amesisitiza kuachwa tabia ya kufanya siasa za udini kwani zinachochea migogoro miongoni mwa madhehebu na jamii.
“Acheni kabisa mambo ya kuingiza udini kwenye siasa, kwani inachochea migogoro miongoni mwetu, hii sio asili ya Tanzania kuwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kwani tumezoea amani, upendo na mshikamano,” amesema.
Askofu wa kanisa Anglicana dayosisi ya Tabora Elias Chakupewa akizungumza wakati wa ibada ya Krismasi leo Alhamis Desemba 25, 2025.
Amesema sikukuu hii ikawe ni sababu ya kudumisha heshima ya madhehebu ya dini na kuacha kugeuza majukwaa ya dini kurushiana maneno yanayoshusha heshima ya dini nyingine au utu wa mtu, kwani sio desturi na mila za Watanzania.
Ameongeza kuwa Tanzania ni taifa la kupigiwa mfano kwa namna lilivyodumisha amani yake na kuwa kimbilio la baadhi ya mataifa ambayo yamekua na migogoro ya muda mrefu,hivyo isiwe rahisi kuichezea amani iliyopo.
“Sisi tuliobahatika kutembea kwenye nchi mbalimbali tunaweza kusimulia vizuri madhara ya machafuko kwani hakuna kinachoweza kufanyika kwa ajili ya maendeleo ya taifa,” amesema.
Kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu wa jimbo hilo, Juda Ruwa’ichi amesema Watanzania wengi hawashabikii haki wala sio wadau wa haki.
Amesema wengi wao kwa ujinga, kwa kurubuniwa au vinginevyo wamekuwa wadau wa amani akiweka msisitizo kuwa pasipo na haki hakuna amani.
Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Juda Thaddeus Ruwa’ichi.
“Sisi tunaoadhimisha Krismasi, kuzaliwa kwa mwokozi tunatakiwa kuwa watu wa haki, wewe mwana Dar es Salaam, Mtanzania je wewe ni mtu wa haki…? Wewe ni mdau wa haki?
“Naomba kuthubutu kusema kwamba Watanzania wengi hawashabikii haki sio wadau wa haki, Watanzania wengi kwa ujinga au kutokujua wanajiadai wadau wa amani,” amesisitiza.
Askofu Ruwa’ichi ameeleza kuwa haki, ugomvi na mtu anayeshabikia amani lakini akiwakumbusha kuwa haiwezekani kuwepo kwa amani bila haki.
“Ewe Mtanzania kama utaka kujigamba kuwa mtu wa amani jitose kupigania haki, jitose kusema kweli, amani na yanayompendeza Mungu,” amesema.
Katika Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Paroko wa Parokia hiyo, Batholomew Mroso, amesema kudai haki na kukataa uovu si chaguo la kanisa bali ni kutimiza msingi wake wa kiimani.
Ameeleza kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni tukio la kipekee lililodhihirisha upendo na ukombozi wa Mungu kwa mwanadamu.
“Nafasi yetu ndani ya Mungu ni kubwa, hivyo lazima tujiulize sisi ni kina nani na kusudi letu ni nini,” amesema, akihimiza waumini wasiwe waoga bali wasimame imara kutetea haki na kukataa uovu.
Padri Mroso amesema Kanisa linapopinga adhabu ya kuua watu hata wenye makosa, linajikita katika misingi ya Kristo aliyezaliwa ili kuleta ukombozi na heshima kwa utu wa mwanadamu.
“Kanisa linapotetea haki kwa kukataa watu kunyongwa, hata kama wana makosa, ni katika misingi hiyo ya Kristo aliyezaliwa kama mwanadamu ili atuletee uhuru na haki,” amesema.
Kuhusu mwaka 2025, amesema umekuwa na matukio mengi yasiyopendeza, hivyo 2026 unapaswa kupita na mambo yake yote mabaya yasahaulike na kuanza ukurasa mpya.
“Ninaamini kila mmoja anatamani huu mwaka upite upesi, ndiyo upite haraka na mambo yake yote,” amesema.
