SIMBA inatarajiwa kuupokea ugeni mzito wa kocha mpya, Steve Barker na wasaidizi wake wikiendi hii kabla ya kuanza safari ya kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, lakini kuna jambo linaloonekana mabosi wa klabu hiyo hawatanii, ni kuhusu msako wa kipa mpya.
Timu hiyo inayoshika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na inayoburuza mkia Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ni moja ya timu 10 zinazoshiriki Kombe la Mapinduzi inayoanza Jumapili ikipangwa Kundi B na Muembe Makumbi na Fufuni zote za visiwani humo.
Hata hivyo, timu hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa timu zilizotwaa Kombe la Mapinduzi ikifanya hivyo mara nne, nyuma ya Azam inayoongoza kwa kutwaa mataji matano, itaenda Zanzibar ikiwa na kipa mmoja tu, Hussein Abel kutokana na Moussa Camara kuwa majeruhi wa muda mrefu, huku Yakoub Suleiman aliyepo na timu ya taifa, Taifa Stars katika michuano ya CAF naye akiumia goti.
Kutokana na hilo kama tulivyoripoti mapema mabosi wa klabu hiyo wameanza msako wa kipa mpya, lakini haikutegemewa kama wapo siriazi kiasi kikubwa kama taarifa hii iliyopenyezwa Mwanaspoti tayari imebisha hodi Mtibwa Sugar kutaka kipa mpya.
Ipo hivi. Kipa namba moja wa Mtibwa, Constantine Malimi ameziingiza timu tatu vitani zikiwania saini yake, huku Simba nayo ikihusishwa kuwa imefanya mawasiliano nayo ili kumnasa dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa wiki ijayo na kufungwa Januari 31 mwakani.
Chanzo cha kuaminika kutoka Mtibwa zinasema klabu hiyo imepokea ofa kutoka timu mbili za JKT Tanzania na Singida Black Stars zinazomtaka Malimi, huku ikielezwa pia Simba nayo imeonyesha nia ya kumtaka japo hawajapeleka ofa yao mezani kwa mabosi wa Manungu.
“Malimi ameziingiza vitani timu mbili hadi sasa ambazo ni JKT Tanzania na Singida BS, hizi ndizo zilizotuma maombi rasmi ya kumhitaji kocha huyo hadi sasa uongozi haujaamua watamtoa au laa,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kutoka Mtibwa kilichongeza;
“Ukiondoa timu hizo mbili, pia Simba imeonyesha nia, ila haijaleta barua rasmi kwani mchezaji huyo bado ana mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hii iliyorejea Ligi Kuu msimu huu.”
Mtoa taarifa huyo alisema Simba inamwona Malimi mwenye clean sheet nne katika Ligi Kuu akishika nafasi ya pili sambamba na Omar Gonzo wa JKT nyuma ya kinara Erick Johola wa Mashujaa mwenye sita hadi sasa kama kipa sahihi kipindi hiki wanasikilizia makipa walio majeruhi wapone.
Hata hivyo, inaelezwa licha ya kumuulizia Malimi, lakini Simba inadaiwa inamsaka pia kipa wa kigeni hata kwa mkataba wa muda mfupi kwa lengo la kumtumia kwa mechi nne za makundi za kimataifa, huku Abel akisikiliziwa kwani alishaanza kuomba kuondoka dirisha dogo kutafuta changamoto mpya.
Chanzo hicho kutoka Mtibwa, kiliongeza, ni mapema sana kwao kuweka wazi watafanya biashara na timu ipi, kwani wanasubiri ripoti ya kocha Yusuf Chipo ambaye ndiye aliyekaa na timu muda mwingi kama atakuwa tayari wao wafanye biashara ya kipa huyo.
“Hatma ya Malima ipo chini ya kocha Chipo, kama ataona sawa sisi tufanye biashara kutokana na kuwa na imani na makipa wengine waliopo tutafanya hivyo lakini kama ataona hakuna haja biashara haitafanyika.”
Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa, Swabri Aboubakar kuzungumzia ofa hizo alisema ni kweli zipo zilizofika rasmi mezani kwao kumhusu kipa huyo, lakini ni mapema sana kuzizungumzia kwani bado hawajafanya uamuzi.
“Ni kweli kuna ofa tumepokea hivi karibuni, si rahisi kuziweka bayana kwa sasa, bado hatujafikia makubaliano, hivyo mambo yakienda sawa kila kitu kitatangazwa, ila kinachotakiwa kufahamika kwa sasa ni Malimi ni mchezaji halali wa Mtibwa na kama kuna timu zinahitaji huduma yake zije mezani kwa mazungumzo na kusifanyike janjajanja,” alisema Swabri.
Kwa misimu minne mfululizo, Simba imejikuta ikiingia sokoni kusajili makipa kutokana na majanga ya majeraha yanayowakumba makipa wao, kwani ilianza kwa Aishi Manula kabla ya kuhamia Azam FC msimu huu, pia kuna Ayoub Lakred aliyerejea Morocco, mbali na Mbrazili Jefferson Luis aliyetemwa timu ikiwa pre season huku Uturuki alipobainika jeraha lake ni la muda mrefu.