SIKU chache baada ya kufahamika kuwa mabosi wa KMC wameafiki kuamuajiri aliyekuwa kocha wa Zimamoto ya Zanzibar, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ ili kwenda kuchukua nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo, kocha huyo inadaiwa ametua na msaidizi kutoka visiwani humo.
Maximo aliachana na kikosi hicho Desemba 6, 2025, baada ya kudumu kwa siku 131, tangu alipotambulishwa, Julai 28, 2025, ambapo kwa msimu wa 2025-2026, aliiongoza KMC katika mechi tisa za Ligi Kuu, akishinda moja, sare moja na kuchapwa saba.
Baada ya Maximo kuondoka, mabosi wa KMC wamefikia makubaliano ya kumuajiri Baresi hadi mwishoni wa msimu huu, huku kocha huyo akitua na msaidizi wake ambaye ni Juma Abdallah Pweka, aliyefanya naye kazi pia katika timu ya Jamhuri ya Zanzibar.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, umeliambia Mwanaspoti Baresi tayari amesaini mkataba wa kukitumikia kikosi hicho na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa, baada ya mchakato wa kumpata Pweka ili awe msaidizi wake kukamilika.
“Mchakato mzima umekamilika na baada ya majadiliano ya muda mrefu hatimaye tumekubaliana na Baresi ili kukiongoza kikosi chetu hadi mwisho wa msimu, malengo makuu tuliyompa ni kuhakikisha timu inabakia Ligi Kuu,” kilisema chanzo hicho.
Mtoa taarifa huyo alisema baada ya Baresi kumpendekeza Pweka ili kusaidiana naye, kocha msaidizi Imani Mwalupetelo aliyekuwa akikifundisha kikosi cha timu za vijana cha KMC atashirikiana nao, hivyo, makocha wasaidizi watakuwa wawili.
Mara ya mwisho kwa Baresi kufundisha timu ya Ligi Kuu Bara, ilikuwa ni maafande wa Mashujaa, ambao kocha huyo aliachana nao Februari 26, 2025, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 3-0, dhidi ya Singida Black Stars.