HUTOKEA mara chache sana kwa wachezaji kupigiana chapuo na hiki kimedhihirishwa na nyanda wa Coastal Union, Wilbol Maseke aliyemtaja kipa wa Pamba Jiji, Yona Amosi kuwa anapaswa kutazamwa kwa jicho la ziada, huku akiweka wazi ana kipaji kikubwa na kama atapata nafasi ya kuitwa timu ya taifa, Taifa Stars itasaidia kumpa uzoefu utakaokuja kuibeba timu hiyo kwa miaka ijayo.
Mbali ya Yona Maseke pia amemtaja kipa wa Yanga, Djigui Diarra kuwa ni sehemu ya makipa ambao amekuwa akiwatazama na kujifunza kutoka kwao huku akisisitiza kuwa ni aina ya makipa wanaocheza mpira kama anaoupenda yeye.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maseke alisema amekuwa akijifunza na kuwatazama makipa wengi amebaini Yona ni kipa bora na mpambanaji ambaye hazungumzwi kama makipa wengine huku akiomba wadau na makocha kumuangalia ili waweze kumpa nafasi ya kupata uzoefu katika timu ya taifa.
“Napenda kujifunza na kutazama makipa ambao wamekuwa wakinipa changamoto ya ushindani Diarra na Yona ni makipa ambao nimekuwa nikiwaangali ni wazuri sana wakiwa langoni wanafahamu majukumu yao. Diarra anapenda kucheza kwa miguu zaidi ya mikono ni kipa wa kisasa na mimi huwa napenda kufanya hivyo.”
“Diarra ni kipa mwenye mafanikio makubwa na anathaminiwa na nchi yake. Anayoyafanya Yanga, anayafanya mara mbili zaidi kwa timu yake taifa ya Mali. Nchi yake inathamini anachokifanya, natamani hilo litokee pia kwa Yona, ni kipa mzuri sana ana kila sababu ya kuitwa Stars.”
Maseke alisema, Yona ukiondoa ubora, namba zake pia zinambeba kuwa sehemu ya kikosi cha Stars kwani kwa misimu miwili mfululizo ameonyesha ubora akiwa na Pamba Jiji akiwa panga pangua kikosi cha kwanza, hivyo anapaswa kupewa heshima yake.
“Mimi siyo msemaji wake wala sio kwa ubaya, wanaoitwa Stars ni wazuri, naye pia anastahili kutokana na namba zake.”