UONGOZI wa Pamba Jiji umekubali yaishe kwa kuafikiana na aliyekuwa beki wa kati wa kikosi hicho, Abdallah Kheri ‘Sebo’, ili kwenda kujiunga rasmi na Singida Black Stars kwa ajili ya kumalizia mkopo wake wa miezi sita uliobaki.
Nyota huyo alijiunga kwa mkopo kwenda Pamba kwa msimu mzima, japo tayari ameitumikia miezi sita na sasa atamalizia msimu huu na kikosi hicho cha Singida, huku uongozi wa timu hiyo ukiangalia mwenendo wake kabla ya kumsajili moja kwa moja.
Sebo aliyetamba na timu za JKU, Zimamoto na Ndanda, baada ya msimu huu kuisha atakuwa amemaliza mkataba wake na Azam, hivyo, atakuwa huru kusaini kokote, jambo linaloipa nguvu Singida kumfuatilia kwa ukaribu ili kuangalia mwenendo wake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji (CEO), Peter Juma Lehhet, alisema baada ya ripoti ya benchi la ufundi ndipo wataamua atakayebakia au kuondoka ndani ya kikosi hicho, japo kwa sasa bado ni mapema zaidi juu ya hilo.
Hata hivyo, licha ya kauli ya Lehhet, Mwanaspoti linatambua Sebo amepewa mkono wa kwaheri na kikosi hicho na tayari amejiunga na Singida, huku suala la mkataba wa moja kwa moja utategemea na kiwango atakachokionyesha kwa miezi sita ijayo.
Mbali na Sebo aliyejiunga na kikosi hicho katika dirisha hili dogo litakalofunguliwa Januari Mosi, 2026, wengine ni mabeki, Abdulmalik Zakaria aliyetokea Mashujaa na Abdallah Said Ali ‘Lanso’ wa KMC.
Abdulmalik aliyejiunga na Mashujaa akitokea Namungo Julai 19, 2024, anamaliza pia mkataba wake na maafande hao mwisho wa msimu huu, japo ameamua kutafuta changamoto mpya na sasa Singida imeinasa saini yake.
Kwa upande wa Lanso aliyejiunga na KMC Januari 13, 2024, akitokea Mlandege, mkataba wake na kikosi hicho cha Kinondoni unafikia tamati Januari 2026, jambo linalotoa nafasi kwa Singida kumsajili bure.
