Dar es Salaam. Licha ya uwepo wa mifumo ya kisasa ya tiketi za kielektroniki na masharti ya kisheria yanayosimamia usafiri wa mabasi ya masafa marefu, changamoto katika utekelezaji wa sheria hizo imeendelea kuchochea ulanguzi wa tiketi, hususan katika vipindi vya mahitaji makubwa ya usafiri kama msimu wa sikukuu.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imebaini ukiukwaji wa taratibu za usajili wa abiria katika baadhi ya mabasi, hali inayosababisha kutokuwapo kwa takwimu sahihi za wasafiri, kuhatarisha usalama wao na kuacha mianya ya upotevu wa mapato kwa wamiliki wa mabasi na Serikali.
Akizungumza Desemba 24, 2025 wakati wa ukaguzi eneo la Msata, mkoani Pwani, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo, amesema mamlaka hiyo imekuta tiketi zenye taarifa zinazokinzana kati ya maandishi ya mkono na yale yaliyosajiliwa kwenye mfumo wa kielektroniki.
“Unakuta tiketi moja ina majina matatu tofauti. Jina lililoandikwa kwa mkono ndilo abiria analoonekana nalo, lakini jina la aliyekata tiketi halipo kabisa kwenye mfumo,” amesema.
Amesema hali hiyo ni hatari endapo ajali au dharura itatokea, kwa kuwa inakuwa vigumu kubaini idadi halisi ya abiria waliokuwapo ndani ya basi pamoja na utambulisho wao.
Kwa mujibu wa sheria, kila basi linapaswa kuwa na nakala tatu za manifesto ya abiria, moja hubaki kituo cha kuanzia safari, nyingine hupelekwa polisi na ya tatu hubaki ndani ya basi.
Hata hivyo, Latra inakiri kuwa utekelezaji wa matakwa hayo bado ni dhaifu katika baadhi ya maeneo.
Katika juhudi za kudhibiti changamoto hiyo, Latra imewataka abiria kutumia majina yao kamili yanayolingana na vitambulisho rasmi kama Nida, kitambulisho cha kura au cha kazi ili kuimarisha usalama na ufuatiliaji wa wasafiri.
“Tunasema wazi, matumizi ya majina yasiyo sahihi yanachochea ulanguzi wa tiketi. Hii inawapa mwanya makondakta au wahusika wengine kukata tiketi kwa bei ya chini au kwa makaratasi bila mmiliki wa basi kujua mapato halisi,” amesema Suluo.
Takwimu za Latra zinaonyesha ukubwa wa changamoto hiyo. Katika kipindi cha Desemba mosi hadi Desemba 22, 2025, jumla ya abiria milioni 2.198 walisafiri nchini, huku miamala ya tiketi ikifikia Sh79 bilioni. Hata hivyo, ni Sh4 bilioni pekee zilizofanyika kwa njia ya mtandao.
Kwa wastani, malipo ya mtandao yalikuwa Sh449 milioni kwa siku, sawa na asilimia 11 tu ya miamala yote, hali inayoonyesha kuwa malipo taslimu bado yanatawala, hivyo kuongeza ugumu wa kudhibiti ulanguzi wa tiketi.
Kwa upande wa wamiliki wa mabasi, changamoto hiyo inaelezwa kuchochewa zaidi na uwepo wa watu wasiokuwa rasmi katika stendi.
Mmiliki wa mabasi ya Happy Nation, Issa Nkya, amesema ulanguzi wa tiketi hauchochewi na wamiliki wa mabasi, bali na wapiga debe na watu wanaoingilia mchakato wa uuzaji wa tiketi.
Amesema wamiliki wamekubali mabadiliko ya mfumo, wameingia kikamilifu kwenye tiketi za mtandao na wanafuata sheria, lakini bado wanapata hasara kutokana na vitendo vya ulanguzi vinavyofanywa na watu wanaojifanya mawakala.
“Latra ilitwambia tukishaingia kwenye tiketi za mtandao, ulanguzi utaisha. Sisi tumeingia, lakini wapiga debe bado wapo palepale stendi,” amesema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus Joseph, amesema kutokutumiwa kwa kitambulisho cha Taifa (Nida) katika ukataji wa tiketi za kielektroniki umeacha mwanya wa walanguzi na wasafiri hewa.
“Bila uthibitisho wa Nida, mtu anaweza kukata tiketi nyingi mtandaoni, asisafiri, halafu tiketi hizo zikarudi kuuzwa stendi kwa pesa taslimu,” amesema.
Amesema suala hilo liliwasilishwa mara kadhaa kwa Latra na pendekezo la msingi likiwa ni kuunganisha mfumo wa tiketi za kielektroniki na Nida ili taarifa za abiria ziwe sahihi na zisizoweza kubadilishwa.
Kwa mujibu wa Taboa, changamoto huongezeka zaidi wakati mtandao unapokuwa haufanyi kazi vizuri, hasa kwa wasafiri wa maeneo ya vijijini, hali inayoonyesha pengo kati ya maendeleo ya teknolojia na mazingira halisi ya wananchi.
“Teknolojia imeenda mbele kuliko mazingira ya wananchi wengi. Ndiyo maana utekelezaji wa sheria na upatikanaji wa Nida kwa kila Mtanzania ni suluhisho la msingi,” amesema.
