Trump aishambulia Islamic State Nigeria

Lagos. Serikali ya Marekani, imefanya mashambulizi kwa kundi la kigaidi la Islamic State (IS) katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.

Hatua hiyo ya Trump, ni utekelezaji wa kile alichokiahidi mwezi mmoja uliopita, aliposema atalazimika kulishambulia kundi hilo la IS kutokana na mauaji ya wakristo wasio na hatia.

Hata hivyo, Serikali ya Nigeria Novemba mwaka huu, ilidai hatua ya kutajwa kuwa nchi inayokiuka uhuru wa kidini kuna upotoshaji ndani yake na kwamba hayana msingi.

Taarifa kuhusu kushambuliwa kwa kundi hilo, imetolewa jana Desemba 25, 2025 na Trump kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Truth Social.

Amesema Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi kadhaa, kauli ambayo baadaye ilithibitishwa na Kamandi ya jeshi hilo barani Afrika (Africom), ikisema lilifanyika Alhamisi kwa ushirikiano na Serikali ya Nigeria katika jimbo la Sokoto.

Katika ujumbe wake, Trump amesema chini ya uongozi wake, Marekani haitaruhusu ugaidi wa Kiislamu wenye misimamo mikali kustawi.

Novemba mwaka jana, Trump ameagiza jeshi la Marekani kujiandaa kuchukua hatua nchini Nigeria ili kukabiliana na makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, bila kubainisha mauaji aliyokuwa akiyarejea wakati huo.

Hata hivyo, madai kuhusu kile kinachodaiwa kuwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo nchini Nigeria yamekuwa yakisambazwa katika miezi ya karibuni na baadhi ya makundi ya mrengo wa kulia nchini Marekani, bila ushahidi usiotiliwa shaka.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, ametoa shukurani kwa ushirikiano na msaada wa Serikali ya Nigeria, kupitia mtandao wa X.

Idara ya Ulinzi ya Marekani baadaye ilichapisha video fupi inayoonekana kuonyesha kombora likirushwa kutoka katika chombo cha kijeshi baharini.

Wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilisema katika taarifa kuwa mamlaka za nchi hiyo zinaendelea kushirikiana kwa karibu na washirika wa kimataifa, wakiwemo Marekani, kukabiliana na tishio endelevu la ugaidi na misimamo mikali yenye vurugu.

“Taarifa hizo za ushirikiano zimewezesha kufanyika kwa mashambulizi ya anga yaliyolenga kambi za magaidi kaskazini magharibi mwa Nigeria,” ilisema taarifa hiyo.

Makundi ya ufuatiliaji wa vurugu yanasema hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Wakristo wanauawa kwa kiwango kikubwa kuliko Waislamu nchini Nigeria, taifa ambalo lina uwiano wa karibu sawa kati ya waumini wa dini hizo mbili.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Yusuf Maitama Tuggar, ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa operesheni hiyo ilikuwa ya pamoja, ikilenga magaidi na kusisitiza kuwa haihusiani na dini yoyote.

Bila kulitaja kundi la IS moja kwa moja, Tuggar amesema operesheni hiyo ilipangwa kwa muda mrefu na ilitekelezwa kwa kutumia taarifa za kijasusi zilizotolewa na upande wa Nigeria.

Waziri huyo hakueleza iwapo mashambulizi yamekoma,  akidokeza hatua hiyo itategemea na uamuzi utakaofanywa na uongozi wa nchi hizo mbili.

Mshauri wa Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, Daniel Bwala, ameliambia BBC awali kuwa, hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya makundi ya jihadi inapaswa kufanywa kwa ushirikiano.

Bwala amesema Nigeria iko tayari kupokea msaada wa Marekani katika mapambano dhidi ya waasi wa Kiislamu, huku akitoa angalizo kuwa Nigeria ni taifa lenye mamlaka kamili.

Amesema makundi hayo hayawalengi watu wa dini fulani pekee, bali yameua watu wa imani zote na hata wasio na dini.

Rais Tinubu mara kadhaa amesisitiza kuwepo kwa uvumilivu wa kidini nchini Nigeria, akieleza changamoto za kiusalama zinaathiri wananchi katika dini na maeneo yote.

Hivi karibuni, Trump aliitangaza Nigeria kuwa nchi yenye mashaka, akidai kuna tishio kubwa la kuwepo kwa Wakristo, akisema maelfu wameuawa bila kuwasilisha ushahidi.

Hadhi hiyo hutumiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na inaweza kusababisha vikwazo dhidi ya nchi zinazohusishwa na ukiukwaji wa uhuru wa dini.

Baada ya tamko hilo, Tinubu amesema Serikali yake iko tayari kushirikiana na Marekani na jumuiya ya kimataifa kulinda raia wa imani zote.

Makundi ya jihadi kama Boko Haram na Islamic State West Africa Province (ISWAP) yamekuwa yakisababisha mauaji na uharibifu Kaskazini Mashariki mwa Nigeria kwa zaidi ya muongo mmoja, yakisababisha vifo vya maelfu ya watu, wengi wakiwa Waislamu, kwa mujibu wa Acled, shirika la kimataifa linalochambua vurugu za kisiasa.

Katika eneo la kati la Nigeria, migogoro ya mara kwa mara pia imekuwa ikitokea kati ya wafugaji, wengi wao Waislamu na wakulima ambao mara nyingi ni Wakristo, kuhusu ardhi, maji na malisho.