MBUNGE LUTANDULA ASHIRIKI BATA LA CHRISTMAS NA WAGONJWA

………….

CHATO

IKIWA ni utekelezaji wa kauli mbiu ya KAZI na BATA kwa wananchi wa Jimbo la Chato Kusini, Mbunge wa Jimbo hilo Pascal Lutandula, ameshiriki chakula cha pamoja na watu wasiojiweza, wagonjwa waliolazwa kwenye kituo cha afya Bwanga pamoja na kutoa zawadi mbalimbali kwa baadhi ya watumishi wa kada ya afya.

Hatua hiyo imelenga kuwapunguzia unyonge na kuungana na wakristo wengine katika kusherehekea sikukuu ya Christmas ambayo huadhimishwa Desemba 25 kila mwaka.

Katika Imani, sikukuu hiyo huwakumbusha wakristo wote duniani kuzaliwa kwa mwokozi wao wa ukimwengu Yesu Kristo na kuhimizana kuishi kwa amani, upendo na ushirikiano. 

Kwa kutambua thamani ya siku hiyo muhimu kwa wakristo waliopo kwenye Jimbo la Chato Kusini, Lutandula akalazimika kuandaa chakula maalumu cha usiku ili kushiriki kula pamoja na makundi hayo.

Akiongea na mwandishi wetu, Lutandula amesema ameguswa kuanza na makundi hayo katika sherehe ya Christmas na kwamba huo ni mwendelezo wa kuyafikia makundi mengine katika Jimbo hilo ili kuungana kwa pamoja katika masuala ya kijamii, kimaendeleo na kisiasa.

Amesema wagonjwa wanahitaji utu, faraja na heshima ili kuwapunguzia unyonge na kwamba hatua hiyo huwasaidia kuhisi wapo pamoja na familia na wapendwa wao katika mambo mbalimbali.

Aidha amegusia umuhimu wa kuwathamini watumishi wa kada ya afya ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa usiku na mchana katika kunusuru uhai wa wagonjwa wanaofika kwenye vituo vya afya wakiwemo wajawazito na watoto wachanga.

Kadhalika kundi la watu wasiojiweza haliwezi kuachwa nyuma kwa kuwa ni sehemu ya jamii ambayo inapaswa kulindwa, kupendwa, kuthaminiwa na kupewa fursa za kuyapambania maisha yao.

Baadhi ya wagonjwa waliolazwa kwenye kituo cha afya Bwanga, wamemshukuru Mbunge wao kwa kuguswa na uhitaji wa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwathamini kwa kuandaa na kushiriki nao chakula maalumu kwaajili ya kusherehekea sikukuu ya Christmas.

Wamemtakia kila la heri katika utumishi wake wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo, huku wakimtaka aendelee kuwa na moyo wa upendo kwa jamii na kuwaletea maendeleo yanayokusudiwa.

Katika hafra hiyo, Mbunge Lutandula amekabidi zawadi mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa pamoja na watumishi wa sekta ya afya ambao baadhi yao wamekabidhiwa pesa taslimu.

                         Mwisho