Dar es Salaam. Wakati Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba akitoa maagizo kila mkoa kuanzisha vitengo vya kuchunguza na kukabiliana na ujenzi chini ya kiwango, wataalamu wa sekta ya ujenzi wamesema hatua hiyo haitoshi wakieleza mambo matano ya kufanya kushughulikia changamoto hiyo.
Wataalamu hao wamesema vitengo anavyovitaja Dk Mwigulu tayari vipo katika mikoa mingi, lakini vinakabiliwa na matatizo kadhaa, yakiwamo upungufu wa wataalamu wa kutosha, kutokujengewa uwezo na kuingiliwa na wanasiasa na hivyo kukosa uhuru.
Changamoto nyingine zinazochangia miradi kutekelezwa chini ya viwango, ni watendaji kukariri bei bila kuzingatia uhalisia wa soko na kuyumba kwa bei za vifaa vya ujenzi.
Kwa mujibu wataalamu hao, mazingira hayo yamesababisha majengo na miradi mingi kujengwa chini ya kiwango, huku lawama nyingi zikielekezwa kwa wakandarasi, ilhali tatizo linatokana na mfumo mzima wa usimamizi katika sekta ya ujenzi.
Desemba 21, 2025, Dk Mwigulu akiwa ziarani mkoani Lindi kukagua miradi ya Serikali, alitoa maagizo ya kuanzishwa kwa vitengo vya kufuatilia hali hiyo kwa kila mkoa, badala ya kusubiri mbio za Mwenge wa Uhuru.
Alisema asilimia 70 ya bajeti ya Serikali inaingia kwenye ununuzi na ujenzi, hivyo ni muhimu maagizo hayo kuzingatiwa ili kulinda fedha zinazotolewa kwa kodi za Watanzania.
“Nimesema kila mkoa uwe na vifaa pamoja na vitengo maalumu vya wataalamu wa kukagua majengo. Bahati nzuri tunaelekea kuandaa bajeti na kazi yao ni kuhakikisha BOQ imezingatiwa na kwamba kilichojengwa ndicho kilichopangwa,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu hali hiyo, Milton Nyerere ambaye ni mhandisi anasema tatizo kubwa linalokwamisha usimamizi wa miradi ya Serikali si kukosekana kwa sheria au miongozo, bali ni upungufu wa wataalamu na Serikali kushindwa kuwajengea uwezo waliopo.
Nyerere anasema Serikali ina wataalamu na sheria za kusimamia wahandisi na ununuzi, lakini idadi ya yao ni ndogo, huku waliopo wakibebeshwa majukumu mengi bila kuimarishiwa mazingira ya kazi.
Akizungumzia agizo la kuanzishwa vitengo maalumu vya usimamizi au ubora, anasema hatua hiyo ni kupoteza muda kwani kila halmashauri ina kitengo cha wahandisi, hivyo kinachohitajika ni kuviimarisha.
“Haiwezekani ofisi iwe na mhandisi mmoja asimamie barabara, hospitali na majengo ya watu binafsi. Kama Serikali inashindwa kuajiri, basi izipe majukumu kampuni binafsi na zikikosea ziwajibishwe,” amesema.
Nyerere ambaye ni mtaalamu wa majengo, anasema badala ya kuanzisha vitengo vipya, Serikali inapaswa kuajiri wataalamu wa kutosha na kuzipatia ofisi vifaa ili kupunguza mzigo wa kazi kwa mtu mmoja.
“Haiwezekani mtu mmoja azunguke mkoa au wilaya nzima kusimamia miradi. Tatizo serikalini ni mtu mmoja kutaka kufanya kila jambo. Kama wanaona ofisi zitajaa, wazipe kampuni kazi,” amesema.
Nyerere amesema taaluma ya uhandisi ina matawi mbalimbali kama ilivyo udaktari, akitoa mfano wa utaalamu wa barabara, majengo, madaraja na usanifu wa ramani, hivyo ni muhimu kila eneo likasimamiwa na mbobezi wake.
Kuhusu ununuzi, amesema tatizo kubwa lipo kwa watu wanaosimamia vitengo bila kuwa wataalamu husika wa miradi.
“Kusema kuanzisha kitengo cha ubora, tatizo liko wapi? Tatizo ni kwamba wanaofanya ununuzi si wataalamu wa ununuzi,” amesema.
Ameeleza mara nyingi watu wanaowekwa kwenye ununuzi ni wa ugavi na ununuzi kwa ujumla, lakini hawana utaalamu wa kiufundi unaohitajika kutathmini miradi ya ujenzi.
“Ni vigumu kupima thamani ya fedha kama si mtaalamu. Jengo likiwa chini ya kiwango maana yake masharti ya mkataba hayakufuatwa,” amesema.
Ametoa mfano wa uzoefu wake aliposhiriki kikao cha ukaguzi wa mradi wa Serikali akieleza kati ya watu zaidi ya 10 waliokuwepo, ni mmoja pekee aliyekuwa na utaalamu na hata yeye hakuwa na uzoefu wa kutosha.
“Nikianza kutoa maelezo hawaelewi. Mwisho wananiambia niongee lugha rahisi. Inafikirisha wanakuja kukagua nini kama hawajui,” amesema.
Amesisitiza katika kila mradi lazima kuwe na mhandisi mshauri ambaye ndiye mwenye mradi na viongozi au wakaguzi wanapaswa kumsikiliza kwani hata mkandarasi humkabidhi ripoti.
Amesema changamoto nyingine ni kucheleweshwa kwa malipo ya wakandarasi, huku mzigo wa lawama ukisukumwa kwao kuficha ukweli, kwamba fedha zilitolewa lakini hazikuwafikia walengwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Fredy Nyenga ambaye ni mhandisi wa barabara, amesema changamoto kubwa inayowakabili wataalamu wa Serikali katika utekelezaji wa miradi ya barabara ni kuingiliwa na wanasiasa wanaolazimisha gharama za miradi zibaki wanavyotaka wao, bila kuzingatia hali halisi ya soko.
Nyenga amesema soko hubadilika mara kwa mara, hivyo haiwezekani gharama za mradi kubaki zilezile kwa kipindi kirefu.
“Kila siku soko linabadilika. Huwezi kusema lami inayojengwa leo itafanana kwa gharama na itakayojengwa mwaka kesho. Fedha hubadilika kila uchao. Mradi uliojengwa mwaka 2020 hauwezi kuwa na gharama sawa na wa mwaka 2025, lakini wanasiasa wanataka ibaki vilevile,” amesema.
Ameeleza kuwa, watumishi wengi wa Serikali hukosa uhuru wa kitaaluma kutokana na hofu ya kusema ukweli, wakihofia kutuhumiwa kuwa wana masilahi binafsi.
“Waliopo serikalini hawana uhuru wa kufanya kazi zao ipasavyo. Wanaogopa kusema ukweli kwa kuhofia kuelezwa kuwa wanataka kunufaika,” amesema.
Nyenga amesema kupanda kwa gharama za mafuta, mabadiliko ya thamani ya fedha na utegemezi wa Dola ya Marekani ni miongoni mwa sababu kuu za gharama za miradi kupanda.
“Gharama ya mafuta ya mwaka 2020 haiwezi kufanana na ya sasa. Fedha yetu si imara, tunategemea Dola ya Marekani. Mabadiliko ya siasa za nje yanaathiri moja kwa moja usafirishaji wa vifaa,” amesema.
Akitoa mfano, amesema kulikuwa na kipindi ambacho dola ilipanda kwa kasi kiasi kwamba waagizaji wa bidhaa walishindwa kupata thamani ileile ya fedha waliyoipanga awali, hali iliyoongeza gharama za utekelezaji wa miradi.
Nyenga amesema kodi za ndani zinazotozwa kwenye vifaa vya ujenzi kama kokoto, mchanga na kifusi zimekuwa zikichangia ongezeko la gharama, huku kila halmashauri ikiweka tozo zake bila uratibu wa pamoja.
“Kila halmashauri inatoza inavyotaka na hakuna anayewajibika au kuuliza maswali,” amesema.
Nyenga amesema ni muhimu wataalamu kupewa uhuru wa kufanya kazi zao kwa kuzingatia hali halisi ya soko, huku akiwataka wanasiasa kuacha kukariri bei zisizokidhi mazingira ya kiuchumi.
“Wanasiasa waache kubana bei na watendaji waache kulazimishwa kubaki kwenye gharama ambazo haziendani na uhalisia wa soko, kwani mzigo humwangukia mtekelezaji wa mradi,” amesema.
