Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa hadi Machi 2024 imelipa jumla
ya shilingi bilioni 949.31 sawa na asilimia 92 ya madeni ya wazabuni wa bidhaa
na huduma pamoja na wakandarasi yaliyohakikiwa kati ya madai yaliyowasilishwa
yenye thamani ya shilingi trilioni 1.03.
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa
Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge
wa Masasi, Mhe. Geoffrey Idelphonce Mwambe, aliyetaka kufahamu hadi sasa
Serikali inadaiwa kiasi gani na wazabuni, wafanyabishara, wakandarasi na walipa
kodi kutokana na huduma, kazi na kodi zilizozidi.
Dkt. Nchemba alisema kuwa kati ya kiasi cha
shilingi trilioni 1.03 cha madeni yaliyohakikiwa hadi machi 2024 shilingi
trilioni 1.02 ni madeni ya wazabuni wa bidhaa na huduma na shilingi bilioni
8.75 ni madeni ya wakandarasi.
Alisema kuwa hadi kufikia Machi 2024, Serikali
ilikuwa inadaiwa jumla ya shilingi bilioni 80.06 ya madeni yaliyohakikiwa
yanayotokana na kodi (VAT Refunds Claims) na imefanya marejesho ya jumla ya
shilingi bilioni 675.1 sawa na asilimia 96 ya lengo kwa kipindi hicho.
Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa
Tabora Mjini, Mhe. Emmanuel Adamson Mwakasaka, aliyetaka kufahamu mpango wa
Serikali wa kuwalipa wastaafu kwa wakati mafao yao, Mhe. Dkt. Nchemba, alisema
kuwa Serikali imeishasimika Mfumo wa Malipo ya Pensheni – TPPS kwa wastaafu
wanaolipwa mafao na Hazina pamoja na kuskani majalada yote ya wastaafu na
kuyahifadhi katika Mfumo wa Malipo ya Pensheni.
Dkt. Nchemba alisema kuwa hatua hiyo imesaidia
mstaafu kupata taarifa na majibu yake kwa haraka wakati wanapotembelea Ofisi za
Hazina Ndogo zilizopo mikoa yote nchini.
Alisema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma
kuhusiana na mafao ya hitimisho ili Mstaafu ajue mfuko sahihi anaopaswa
kulipiwa na aina ya mafao atakayostahili kulipwa.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba
(Mb) akijibu maswali bungeni jijini Dodoma ya Mbunge wa Masasi, Mhe. Geoffrey
Idelphonce Mwambe, aliyetaka kufahamu hadi sasa Serikali inadaiwa kiasi gani na
wazabuni, na swali la Mbunge wa Tabora Mjini, Mhe. Emmanuel Adamson Mwakasaka,
aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwalipa wastaafu mafao yao kwa
wakati.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-
Wizara ya Fedha)