Dodoma. Unawaza kuhusu nyumba ya kulala wageni? Kwa wengine siyo, chini ya mtende kando ya barabarani, tena mbele ya soko, watu wanamaliza tamaa zao za mwili na kuondoka.
Ni vigumu kuamini, lakini ndiyo ilivyo. Mtende ulio barabarani unatumiwa na makahaba kumalizana na wateja zao.
Saa 3:49 asubuhi anaamka mwanadada mweupe aliyejiremba. Anavaa gauni kisha anajipekua kifuani, anatoa noti, kwa mbali inaonekana ni Sh5,000. Anabeba chupa ndogo nyeupe yenye kimiminika na kuiweka mdomoni.
Bila hofu anafungua shuka mbili chafu zilizofungwa mfano wa pazia, anainama kuotoka kondomu iliyotumika. Anagida kimiminika chake kisha anaondoka huku watu wakimtazama.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa siku tatu, usiku na mchana umebaini eneo hilo la mtende linatumiwa na makahaba kufanya biashara ya kuuza miili yao.
Ni mbele ya Soko la Sabasaba, jijini Dodoma. Upande mmoja kuna kibao cha Chuo cha Fedha Kampasi ya Dodoma na mwingine kingine kinachoonyesha kivuko cha watembea kwa miguu.
Nyakati za mchana bajaji ziendazo Kikuyu husimama eneo hilo.
Chini ya mti huu pana harufu kali ya mikojo, kuna vichungi vya sigara, yako mabaki ya kondomu zilizotumika navipande vya maboksi yanayotumika kama magodoro.
Usiku eneo hili la mtende hufungwa vipande vya mashuka kama pazia na shughuli za ukahaba hufanyika usiku kuanzia saa tatu baada ya watu kupungua sokoni Sabasaba.
Biashara hii ambayo ni kinyume cha sheria nchini Tanzania, huendelea hadi saa 11:00 alfajiri watu wanapoanza kupita kwa wingi.
Hata hivyo, baadhi ya wahusika hujikuta wakiamka hadi saa mbili asubuhi kama ilivyojitokeza Jumatano ya Desemba 24, 2025, aliposhuhudiwa mmoja akiamka eneo hilo.
“Hapo halali mmoja, wanakuja kwa kuachiana zamu, kwa hiyo hizo kondomu unazoziona hazikutumika kwa mtu mmoja, sema huyo kachelewa kuamka ndiyo maana anawajibika kuzitoa na kwawao ina maana anafanya usafi hapo,” anaeleza dereva wa bajaji ambaye hakutaka kujatwa jina.
Baadhi ya madereva wanasema mara nyingi huegesha vyombo vyao vya usafiri kwenye eneo hilo hadi usiku.
Inaelezwa nyakati hizo wanawake na wanaume hupishana kuuelekea mtende huo, uliopo karibu mtaro.
Mashuhuda hao wanaeleza kulingana na mazingira ya eneo hilo, baadhi ya maeneo ya mwili huwa nje watu wanapokuwa wakiendelea na shughuli hizo.
Eneo hilo lenye mtende, lina upana wa takribani hatua mbili za miguu na urefu wa hatua tatu kabla ya barabara ya lami itokayo Tanesco kwenda mitaa ya Mwananchi na TBC.
Kwa mujibu wa ufuatiliaji wa Mwananchi, awali shughuli hizo za ukahaba zilifanyika kwenye jumba lililotelekezwa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Lakini, baada ya kukarabatiwa na kupata watu wa kuishi, walihamishia kambi mita chache kutoka hapo.
Kwenye michongoma iliyo jirani na jumba hilo karibu na baa mbili maarufu Mtaa wa Uhindini pia shughuli hizo inafanyika.
Mbali na eneo hilo, maeneo mengine yanayotajwa kutumika kwa ukahaba ni Mtaa wa Airport nyuma ya msikiti, Sabasaba na eneo la Ipagala jirani na makaburi.
Inaelezwa baadhi wanatoka upande wa pili wa barabara eneo maarufu la Chako ni Chako ambako inaelezwa biashara imepungua kutokana na uchache wa watu, pia ikidaiwa waendao hapo hawana fedha.
Ili kuzungumza na mmoja wa makahaba hao, lazima utoboke mfuko. Baada ya kumlipa Sh3,000, mmoja wao anaeleza namna wanavyofanya biashara, akiwataja adui wao mkubwa kuwa ni polisi wa doria.
“Ukinipiga picha hata kwa siri nakupasua na chupa halafu nasema ulinibaka, ole wako, sisi kilichotuleta hapa ni hizi baa kubwa kama unavyoona watu wanajazana,” anasimulia kwa kujiamini.
Mwanadada huyo anayesema alimaliza masomo ya kidato cha nne, anasema wanapambana na anachokiita maisha ya usasa.
“Wateja wakubwa ni wanaume ambao wamehamia huku wakifanya kazi mbali na familia zao, kwetu sisi ndiyo fursa na tunawapiga hasa. Ukienda ‘gesti’ unaishia kupewa Sh10,000 lakini unatumikishwa hadi asubuhi, tunawataka watumie muda mfupi ndiyo tunakwenda pale kwenye mtende,” anasimulia majira ya saa nne asubuhi, akionekana mtu aliyelewa.
Haogopi kutaja wilaya anayotoka kuwa ni Bahi ingawa hapendi kijiji chake kiandikwe licha ya kukitaja na anakiri wastani wa kipato kwa siku ni Sh20,000 hadi Sh35,000 kwa malipo ya Sh5000 hadi Sh10,000 wanayolipwa kila wanapokubaliana na mteja mmoja ambaye mkataba ni kutozidi dakika 15.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Soko la Sabasaba, Kombo Kombo, anakiri tabia hiyo ipo na mara nyingine wamekuwa wakishuhudia mambo mengi aliyoyaita ya hovyo yakifanyika.
Hata hivyo, anasema kila wakati wanapotoa taarifa kwa mamlaka za Serikali wanaona kama zimekaa kimya.
“Ni kweli hayo mambo na mengine yapo hapa sokoni, kuna maeneo wanajibanza na wanaharibu sifa njema ya soko letu. Sisi tunatoa taarifa kila wakati kwa mamlaka husika, lakini tunaona wako kimya, tusaidieni kupaza sauti watusikilize,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema hana taarifa rasmi kuhusu hali hiyo akaahidi atafuatilia kuona nini kinatendeka na hatua zitachukuliwa.
“Asante kwa kunipa taarifa, naahidi kufuatilia kuhusu jambo hilo kwa haraka na kudhibiti halafu mtapata taarifa,” amesema.
Hata hivyo, mwandishi hakuweza kupata kauli ya Jeshi la Polisi, kwani kwa siku tatu mfululizo simu ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, imekuwa ikipokelewa na mtu anayejitambulisha kuwa msaidizi wake, ambaye amekuwa akielekeza maswali hayo yaulizwe kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya.
Mwandishi alipowasiliana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya kwa njia ya simu, aliipokea lakini akaeleza kuwa yupo eneo lenye mvua kubwa, hali iliyofanya mawasiliano kuwa magumu.
Baadaye, mwandishi alipiga tena simu ya Kamanda wa Polisi na kama ilivyokuwa awali, ilipokewa na msaidizi wake, ambaye aliahidi kumpigia mwandishi baadaye. Ahadi hiyo ilitekelezwa muda mfupi baadaye:
“Ndugu mwandishi, Afande RPC amepokea maoni yako na ametoa maagizo kwa Afande OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) tumpe siku tatu mtaona jambo hilo likikomeshwa na halitajirudia, sijui kama kuna lingine zaidi ya hapo,” amesema Msaidizi wa RPC.
