Serikali yataka ugawaji vizimba Kariakoo uzingatie bei halisia

Dar es Salaam. Serikali imeutaka uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo kuhakikisha upangishaji wa vizimba na vyumba katika soko hilo, unazingatia bei halisi ili kulinda maslahi ya wafanyabiashara na kuwanufaisha walengwa.

Kauli hiyo ya Serikali, inakuja katikati ya malalamiko ya wafanyabiashara wa soko hilo, wanaolalamikia danadana za ufunguzi wa soko tangu ujenzi wake ulipokamilika mapema mwaka huu.

Hata hivyo, uongozi wa soko hilo, umesema Januari mwakani ndipo soko hilo litafunguliwa na kuanza kufanya kazi, huku upangaji wa wafanyabiashara na ukarabati wa baadhi ya maeneo zikiwa sababu za kuchelewa kwa ufunguzi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, wakati wa ziara yake sokoni hapo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Rizik Shemdoe amesema Serikali ilitoa fedha za ukarabati ili kuwasaidia wafanyabiashara.

Amesema Sh28 bilioni zilitolewa kuhakikisha ukarabati unafanyika na kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira bora, hivyo hakutakuwa na nafasi ya vitendo vya udalali au upangishaji usiozingatia misingi ya haki.

“Serikali ilitoa fedha hizi kwa dhamira ya kumsaidia mfanyabiashara, bei za upangishaji wa vizimba na vyumba lazima ziendane na hali ya soko ili kuepusha malalamiko na kuondoa mianya ya watu wachache kujinufaisha,” amesema Profesa Shemdoe.

Amesema fedha hizo zimetolewa kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alilenga kuhakikisha wafanyabiashara wa soko hilo wanafanya biashara katika mazingira salama ya kisasa na yenye tija.

Ili kupunguza migogoro na malalamiko yanayoendelea kujitokeza, Profesa Shemdoe ameutaka uongozi wa soko hilo kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara waliokuwepo awali katika soko hilo kabla ya kuwapa nafasi wapya.

“Ni muhimu ili kulinda haki za wafanyabiashara wa awali na kuhakikisha urejeshwaji wao unafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa,” amesema.

Profesa Shemdoe ameonya vitendo vya kumiliki zaidi ya kizimba au chumba kimoja katika soko jipya, hasa kwa wale waliokwishapata nafasi kupitia mfumo wa Tausi, akisisitiza hilo haliruhusiwi.

Ameuelekeza uongozi wa soko kuhakikisha hakuna mtu anayepewa kizimba au chumba kinyume na utaratibu wakati bado wapo wafanyabiashara halali wanaosubiri kupangiwa.

Akizungumzia suala la usalama wa biashara, Profesa Shemdoe ameutaka uongozi wa soko kuhakikisha majengo yote yanakatiwa bima, sambamba na kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa bima kwa biashara zao.

“Ni muhimu katika kulinda mitaji ya wafanyabiashara dhidi ya majanga yanayoweza kujitokeza, ikiwemo ajali za moto ambazo hapo awali zimesababisha hasara kubwa katika soko hilo,” amesema.

Wakati waziri akitoa kauli hiyo, Amani Munuo mfanyabishara wa soko la Kariakoo, amelalamikia kuchelewa kufunguliwa kwa soko hilo kwani kumesababisha changamoto ya barabara nyingi sokoni hapo kutopitika.

Sababu ya kutopitika kwa barabara hizo, amesema ni wafanyabishara waliokuwa kwenye soko hilo, walihamishia biashara zao kwa muda katikati ya barabara wakisubiri soko lifunguliwe.

“Pia, soko hili lilikuwa kivutio ndani na nje ya nchi, sasa kufungwa kwake kwa muda mrefu mapato yanazidi kushuka. Wapo wafanyabiashara walioamua kutulia wakiamini ndani ya muda mfupi soko litafunguliwa sasa wamekula mitaji yao kutokana na soko kuchelewa kufunguliwa,” amesema.

Kaimu Katibu Tawala Msaidizi (Miundombinu) wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aman Mafuru amesema ukarabati wa Soko la Kariakoo umezingatia uwekaji wa miundombinu ya kisasa.

Miundombinu aliyoitaja ni mifumo ya kukabiliana na ajali za moto, lifti za kubeba bidhaa, wafanyabiashara, wanunuzi na maboresho ya usalama kwa ujumla.

Amesema miundombinu hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa biashara na kuimarisha usalama wa mali na watu ndani ya soko hilo.

Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Mwinga Luhoyo amesema upangaji wa maeneo kwa wafanyabiashara ulikuwa shirikishi.

Amesema viongozi wa wafanyabiashara hao walishirikishwa, wameshajaza mikataba na imeingizwa kwenye mfumo wa Tausi tayari kwa kuanza biashara soko litakapofunguliwa.