Sikukuu za kimila zilivyotumika kupata wenza

Shinyanga. Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mikoa ya Kisukuma, Mtemi Kidola Charles Njange, amesimulia namna ambavyo sikukuu za kimila, ikiwemo Krismasi na sikukuu ya mavuno, zilivyokuwa zikitumika kuwaunganisha vijana wa kike na wa kiume katika kutafuta wenza wa maisha.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Mwananchi kuhusiana na maadhimisho ya sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya, Mtemi Njange amesema, jamii ilikuwa ikijumuika kwa pamoja katika hali ya mshikamano mkubwa.

Ameeleza kuwa watu walishiriki chakula, kucheza ngoma za asili na kukesha hadi usiku wa manane wakisubiri kuipokea sikukuu, hatua iliyokuwa ikiimarisha umoja, mahusiano ya kijamii na kudumisha mila na desturi za jamii.

“Baada ya kukesha kusubiri sikukuu, wakati wa kurudi nyumbani vijana wa kiume walisubiria mabinti njiani na kila mtu kujichagulia. Iliitwa chagulaga kwa kabila la Kisukuma, baada ya hapo vijana walipelekana kwa wazazi na wao pia walichukua hatua ya kuanza kuchunguza familia hiyo.

“Mzazi akiona binti yake hajachukuliwa na kijana inaonekana kama ni mkosi, na hivyo anachukua hatua ya kwenda kumuogesha dawa za kienyeji kuondoa nuksi na kumsafisha,” ameongeza.

Pia, amesema kuwa: “Hasa wazazi walichunguza kama kuna magonjwa ya kurithi mfano ukoma au kuna tabia za kishirikina, ni wachapakazi na mengineyo mengi, ambapo kama familia itakutwa na hata kimoja kati yao wazazi hawakuruhusu mahusiano hayo” amesema.

Mtemi Njange amesema kuwa katika sikukuu za kisasa, mshikamano wa kijamii uliokuwapo zamani umepungua kwa kiasi kikubwa.

Amebainisha kuwa ngoma za asili, ambazo zamani zilikuwa chombo cha kuimarisha umoja na mshikamano wa jamii, kwa sasa zimegeuzwa kuwa shughuli za kibiashara, jambo linalopunguza thamani yake ya kijamii na kitamaduni.

“Zamani mtu yeyote alitazama ngoma bila malipo lakini kwa sasa limekuwa suala la kibiashara, mtu analipia ndio anaingia kutazama ngoma, ule mjumuiko na ushirikiano haupo tena kwa sababu kwa sasa kijana akimchukua binti anaonekana atamfanyia ukatili na hii ni sababu ya kumomonyoka kwa maadili,” ameongeza.

Akizungumza kwa mtazamo wa vijana, Maganga Nzengo amesema mabadiliko ya maisha ya kisasa ndiyo yamechangia kwa kiasi kikubwa kubadilika kwa mienendo na mahusiano ya kijamii.

Nzengo ameeleza kuwa maendeleo ya teknolojia, mitandao ya kijamii, mabadiliko ya uchumi na mtindo wa maisha yamewafanya vijana wengi kuishi kwa kujitegemea zaidi, tofauti na zamani ambapo jamii ilikuwa karibu na kushirikiana kwa pamoja katika kila tukio la kijamii na la kitamaduni.

Kwa upande wake, Juma Kayogela amesema kuna tofauti kubwa kati ya maisha ya zamani na ya sasa.

Amefafanua kuwa hapo awali watu waliishi kwa kuzingatia mila, desturi na mshikamano wa kijamii, huku sikukuu na sherehe zikitumika kama fursa ya kuimarisha umoja na mahusiano.

Akizungumza kuhusu mahusiano ya kisasa kati ya vijana, Halima Ng’wanidete amesema wengi wa vijana hupata wachumba wao wakiwa shuleni, jambo linaloonyesha jinsi mahusiano ya mapenzi yanavyopatikana mapema katika maisha ya shule na jinsi shule zinavyokuwa chimbuko la kuanzisha uhusiano wa kimapenzi.

Kwa upande wake, Magdalena Damian amesema kuwa katika nyakati hizi, uchaguzi wa wanaume kwa msichana ni huru na wa hiari.