HAMAD FURAHISHA AMETUFURAHISHA


 ::::::::

Bondia wa ngumi za kulipwa Hamad Furahisha raia wa Tanzania usiku wa kuamkia leo alikua kwenye ubora wake wa hali ya juu dhidi ya Mmalawi Hanock Phiri.

Kuanzia raundi ya kwanza hadi ya sita Furahisha alicheza vizuri lakini kuna namna alitaka kubishana na Phiri katika aina yake ya mchezo ambao uliwapa shida mabondia kadhaa wa watanzania aliowahi kucheza nao.

Furahisha alibadilishana mikono na Phiri kitendo ambacho kingezidi kuwa changamoto kwake kwasababu huyu Mmalawi sio bondia wa kubeza

Ilipofika raundi ya sita Furahisha alibadilisha ‘game plan’ yake ya kusimama na kupigana hatimaye akawa anapiga ana ‘score’ kisha anatembea kitendo ambacho Phiri kilimvuruga kuanzia raundi hiyo hadi mwishoni mwa pambano ambapo alipokea ngumi nyingi ambazo alishindwa kuzifanyia ‘counter punch’

Licha ya Phiri kupoteza pambano hili lakini sio bondia wa kubeza na laiti kama angekutana na mabondia wavivu wa mazoezi basi wangeaibika.

Wakati mwingine makocha wa Furahisha wanatakiwa kumkumbusha Furahisha ni hatari kupigana kisha kumpa mgongo mpinzani wako hata kama una lengo la kutembea ulingoni ili kulinda ulichopata ila angalia aina ya utembeaji wako.

Nilisema hili ni pambano ambalo ni tobo kwa Furahisha ambalo linaenda kumuweka kwenye ramani nzuri ya mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini.

Phiri amepigwa na amekubali kuwa amepigika.

“Leo haikua siku yangu na nampongeza mpinzani wangu,”amesema Phiri.

Furahisha amesema maandalizi ndio chachu ya ushindi huo.

HONGERA HAMAD FURAHISHA